Home Habari SIKU ZA OMOG SIMBA ZAHESABIKA

SIKU ZA OMOG SIMBA ZAHESABIKA

1041
0
SHARE

NA SAADA SALIM

SIKU tano baada ya kutoka sare na Azam FC, uongozi wa klabu ya Simba umeamua kumpa mechi tano kocha mkuu wa timu hiyo, Joseph Omog, kubadili mwenendo wa matokeo ya timu na kuhakikisha timu inapata ushindi na kucheza mpira unaovutia.

Simba ilianza vizuri mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa kuibamiza Ruvu Shooting mabao 7-0, lakini ikasimamishwa na Azam Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Chamazi Complex, jijini Dar es Salaam katika mechi ya pili na kulazimishwa suluhu ya bila bao, huku safu yake ya ushambuliaji ikionekana kuwa butu.

Kitendo cha timu hiyo kulazimishwa suluhu, kimeufanya uongozi wa Simba chini ya Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo kumtaka Omog ahakikishe timu yake inashinda mechi nne zijazo ikiwemo dhidi ya Mwadui FC, watakaocheza Septemba 17, mwaka huu kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Mechi nyingine zijazo ni dhidi ya Mbao FC ambapo Simba watakuwa wageni katika mchezo huo utakaopigwa Mwanza, dhidi ya Stand United, utakaochezwa Shinyanga na Mtibwa Sugar utakaopigwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Taarifa za uhakika zilizolifikia DIMBA kutoka kwa kigogo wa Simba, zinadai kwamba Kamati ya Utendaji ya Simba ilikutana hivi karibuni na kujadiliana mwenendo wa timu yao na kutoa maelekezo kwa benchi la ufundi linaloongozwa na Omog kuhakikisha wanashinda mechi tano ingawa walianza na suluhu dhidi ya Azam FC.

Kigogo huyo ameliambia DIMBA Jumatano kuwa timu yao hiyo iliambulia pointi mmoja katika mchezo huo na sasa wanaendelea na hesabu yao, huku mechi dhidi ya Mwadui ikiwa ni mchezo wa pili katika ya michezo mitano ambayo alipewa Omog kuhakikisha wanashinda.

“Ni kweli Omog amepewa mechi tano kuhakikisha anaibuka na ushindi, ambapo mechi ya Azam wametoka sare pia tunaendelea na mpango huo kuhakikisha timu inafanya vizuri katika mechi hizo na zingine ili yasitukute yaliyotukuta  msimu uliopita,” alisema.

Kwa mujibu wa kigogo huyo, hicho ni kipimo kwa kocha huyo kuhakikisha wanafikia malengo yao ya msimu huu, ambapo wanahitaji kutwaa ubingwa kwa udi na uvumba.

Alisema Omog akishindwa kufikia mikakati waliyomuwekea, kocha huyo atalazimika kuondoka na kuachia nafasi wengine kuendelea kukinoa kikosi cha timu hiyo.

Alisema tayari uongozi umeshaanza mazungumzo na makocha mbalimbali akiwemo kocha wa timu ya USM Alger ya Algeria, Mbelgiji Paul Put pamoja na kocha wa zamani wa Wekundu hao raia wa Serbia anayeinoa klabu ya Ferencvárosi Torna Club ya Hungary, Goran Koponovic.

“Omog akishindwa kufikia haya tuliyompa atusamehe, kwani tayari mlezi wetu Mohammed Dewji (MO) amametuhakikishia kwamba tutafute kocha mwenye kufikia malengo ya Simba na atamlipa kiasi atakachokihitaji,” alisema kigogo huyo.

Omog mwenyewe anaonekana kulifanyia kazi suala la kufanya vizuri kwa timu ambapo katika mazoezi ya jana kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, alikuwa akiwapa vijana wake mbinu maalumu za kusaka mabao.

Katika mbinu hizo ambazo zilikuwa mbili, mojawapo ilikuwa ni kusaka mabao kupitia katikati na nyingine kupitia pembeni, ambapo mipira ilikuwa ikianzia kwa beki wa kati, Salim Mbonde ambaye huipenyeza kati kwa kiungo mmojawapo kati ya Jonas Mkude, Said Ndemla au James Kotei ambaye hupiga pembeni kwa Mghana Nicholas Gyan ama Shiza Kichuya ambao huirudisha kati kwa Ndemla au Kotei kisha kupenyezwa pembeni kwa mabeki, Shomari Ally au Erasto Nyoni kwa ajili ya kupiga krosi zinazosubiriwa na mastraika, Emmanuel Okwi ama John Bocco.

Omog alisema kikosi chake kipo vizuri na sasa wameweka mikakati kuhakikisha timu inashinda idadi kubwa ya mabao kwa kuanzia bao 3 na kuendelea, ambapo wataanzia katika mchezo wao na Mwadui.

“Kikosi kipo vizuri tunaendelea na mazoezi, tayari tumeshawaeleza washambuliaji na kikosi kwa ujumla tunahitaji ushindi wa idadi nyingi ya mabao kuanzia matatu na kuendelea kwa kila mechi,” alisema.

Kocha huyo alisema kukosa ushindi katika mchezo wa Azam haikuwa bahati yao pia kutokana na wachezaji wa timu zote mbili kukamiana, hali iliyopelekea kushindwa kupatikana kwa matokeo mazuri.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here