SHARE

NA SAADA SALIM,

HAPA KAZI TU! Hivi ndivyo unavyoweza kuizungumzia Simba ambayo haijachukua taji la Ligi Kuu Bara tangu ilipofanya hivyo msimu wa 2011-2012. Misimu kama minne mfululizo imekuwa ikizisindikiza Yanga na Azam FC.

Msimu huu upepo kama umegeukia kwao, imemaliza duru la kwanza wakiwa kileleni na pointi 35 na kuendelea kung’ang’ania katika nafasi hiyo hadi sasa ikiwa na pointi 45, ila huenda ikakumbana na ugumu kuendeleza kasi hiyo  katika mchezo wao dhidi ya Azam mwishoni mwa wikiendi hii.

Mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, kati ya Simba dhidi ya Azam, utakuwa ni mchezo wa kisasi kutokana na Wekundu hao wa Msimbazi kutokubali kufungwa hasa wakifikiria kichapo cha bao 1-0 katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar.

Simba inaingia kambini kesho Ndege Beach eneo la Mbweni, Dar es Salaam kujiandaa na mchezo dhidi ya Azam, ambapo wachezaji wote wameingia kambini kujiandaa na mchezo huo utakaopigwa Jumamosi.

Wekundu hao wa Msimbazi wanataka kulipiza kisasi kwa Azam ili kufuta machungu ya kufungwa wakati wa fainali ya Kombe la Mapinduzi na kupata pointi tatu muhimu zitakazowabakiza katika nafasi ya juu waliyokuwepo kwa sasa.

Omog ameliambia DIMBA Jumatano kwamba lengo lake kubwa ni kuhakikisha timu yake inafanya vizuri ili kufikia malengo ya kurejesha furaha kwa Wanasimba kwa timu hiyo kutwaa taji la Ubingwa.

Alisema licha ya kufanya maandalizi ya ligi na kuziheshimu timu zote na licha ya siku chache zilizopita kukutana na Azam, bado ana imani kikosi chake kipo vizuri huku akihitaji pointi muhimu katika mchezo huo.

“Sitapuuza timu yoyote tutakayokutana nayo, nawaheshimu Azam kwani walitufunga Mapinduzi, nimeyafanyia kazi mapungufu kwani mchezo huu utakuwa wa ushindani mkubwa kwani hatutakubali kufungwa mara ya pili na mpinzani wetu,” alisema Omog.

Naye kocha wa Azam, Iddy Nassor ‘Cheche’, amesema licha ya kuifahamu Simba na kuifunga katika Kombe la Mapinduzi, bado anaingia kwa tahadhari na kuhakikisha wanafanya vizuri.

“Nimewaona Simba juzi walipocheza na Polisi Dar wamebadilika, hivyo  nimelazimika kubadili mbinu kwa ajili ya kuwakabili wapinzani hao ili kupata pointi muhimu,” alisema Cheche.

Wakati huo huo, Mtendaji Mkuu wa Azam, Saad Kawemba, alisema suala la kibali cha kocha wao Mromani, Aristica Cioaba, kinaendelea vizuri baada ya kufuata taratibu zote ambapo wanasubiri agizo la Serikali juu ya kumruhusu kocha huyo kuanza kazi.

Wakati huo huo mashabiki wa Simba huenda ikawa ni habari njema kwao baada ya straika wao machachari, Mohamedi Ibrahim (MO) aliyekuwa majeruhi kuanza mazoezi mepesi jana katika Uwanja wa Boko Veteran. MO ni mmoja ya mastraika wa kutegemewa wa Simba ambaye aliumia hivi karibuni na kulazimika kukaa nje ya uwanja kwa wiki mbili.

Katika hatua nyingine, mashabiki wa Simba jana walimvamia meneja wa timu hiyo, Mussa Hassan ‘Mgosi’ kutaka kujua nini hasa tatizo linalowakabili mastraika wa timu hiyo kufunga mabao machache tena kwa tabu.

Tukio hilo lilitokea jana wakati Simba ikijifua katika uwanja wa Boko Veteran ambapo Mgosi alilihakikishia benchi la timu la hiyo limeshabaini tatizo na tayari wameshalifanyia kazi na shughuli wataiona kwenye mchezo dhidi ya Azam.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here