Home Habari SIMBA HATUPOI

SIMBA HATUPOI

1624
0
SHARE

NA SAADA SALIM

*Mbelgiji awafariji wachezaji sakata la MO

*Awafua saa 6 juani kuifyekelea mbali Stand

LICHA ya Simba kupitia kipindi kigumu sana kwa mashabiki na wanachama baada ya kutekwa kwa mwekezaji na mwanachama maarufu wa klabu hiyo, Mohammed Dewji ‘Mo’, Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Patrick Aussems, ametoa neno la faraja.

Ilikuwa ni siku ya Alhamisi Oktoba 11, 2018, siku ambayo Wanasimba na Watanzania hawataisahau, kufuatia tukio la kutekwa kwa Mo Dewji, ambaye pia ni mwekezaji mkuu katika klabu hiyo.

Mpaka sasa tukio hilo bado linapasua vichwa vya ndugu, jamaa, Wanasimba pamoja na Watanzania kwa ujumla, wakitaka kujua hatima ya mfanyabiashara huyo kama atapatikana akiwa salama au la.

Tukio la juzi ambapo familia ya mfanyabiashara huyo ikiongozwa na baba wa MO, Ghulum Dewji pamoja na Msemaji wa Familia Azim Dewji kutangaza dau la Sh bilioni moja kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa zitakazowezesha kupatikana kwa mfanyabiashara huyo, zimezidisha hofu miongoni mwa Watanzania juu ya kupatikana kwa mpendwa wao.

Hata hivyo, licha ya kupitia kipindi hicho kigumu, Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Mbelgiji Patrick Aussems, amewaambia mashabiki wa Wekundu hao wa Msimbazi kwamba wajitokeze kwa wingi Jumapili ili waone jinsi timu yao itakavyotoa kipigo kwa Stand United.

Wekundu hao wa Msimbazi, watawakaribisha Stand United, mchezo utakaochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, ambapo Mbelgiji huyo amesema hakuna cha kupoteza zaidi ya kutafuta pointi tatu.

Mbelgiji huyo aliyasema hayo jana baada ya kumalizika kwa mazoezi ya nguvu yaliyofanyika Uwanja wa Boko Veterani, kujiandaa na mchezo huo dhidi ya Stand United.

“Mpaka sasa niseme tu kwamba tunaendelea vizuri, wachezaji wangu wanajituma na nimekuwa nikikaa nao mara kwa mara ili kujua tunafanya nini katika michezo yetu inayokuja.

“Kila mmoja anajua kwamba tupo kwenye wakati mgumu (baada ya kutekwa kwa Mo), lakini hilo halitasababisha kufanya vibaya na badala yake tutahakikisha tunaendelea kushinda.

“Unajua Mo ni mhimili wa klabu hii, lakini pia ni mfanyabiashara mkubwa hapa nchini, hivyo tukio la kutekwa kwa kipindi kirefu sasa linaumiza wengi, lakini nimewaambia wachezaji wangu tupambane ndani ya uwanja,” alisema kocha huyo.

Katika hatua nyingine, Aussems ameamua kuja la `Plan B` kwa mastraika wake kuhakikisha wanafanya vizuri na kupata mabao mengi zaidi ya yale waliyopata msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Simba ilimaliza msimu ikiwa ni mabingwa kwa kujikusanyia pointi pointi 69, wakifunga jumla ya mabao 62, huku Emmanuel Okwi akiibuka mfungaji bora, akipachika mabao 20.

Alisema kwa sasa amekuwa makini kuhakikisha anaisuka safu yake ya ushambuliaji ili kupachika mabao mengi zaidi tofauti na michezo iliyopita, ambayo ushindi mkubwa ilikuwa wa mabao 3-1 dhidi ya Mwadui FC.

“Ukiangalia safu ya ushambuliaji, kuna wachezaji wazuri na wengi ambao wanaweza kufanya mambo makubwa kwenye timu, ila ni jambo la kusubiri tu wakati kuweza kuwa katika ubora wao, hiki ndicho tunachopambana nacho kwamba wafunge mabao mengi zaidi,” alisema.

Katika michezo saba ambayo Simba wamecheza, wamefunga mabao manane, ambapo Meddie Kagere amefunga mabao manne, John Bocco mawili, huku Emmanuel Okwi na Shiza Kichuya kila mmoja akiwa na bao moja.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here