SHARE

NA SAADA SALIM


MAKALI safu ya ushambuliaji ya Simba hayajawahi kumuacha mtu salama iwe mechi ya Ligi au kirafiki.Unajua kwanini.

Ni kile kilichotokea jana uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwa John Bocco kuwaongoza wenzake kuiadhibu bila huruma AFC Leopard ya Kenya kipigo cha mabao 4-2 ukiwa ni mchezo wa kirafiki wa kimataifa.

Wenyeji Simba waliuanza  mchezo huo kwa kasi ambapo dakika ya 12 ya mchezo Mohamed Hussein Tshabalala nusura aiandikie timu hiyo bao baada ya kufumua shuti la mbali lakini likadakwa na kipa AFC Leopard, Jairus Adira.

Bocco ndiye aliyeanza kuzindua karamu ya mabao ya Simba dakika 13 akiunganisha kwa kichwa krosi tamu ya beki Shomari Kapombe na kuandika bao la kuongoza.

Kama siyo kuchelewa kufanya maamuzi kiungo Hassan Dilunga wa Simba aongeze bao la pili dakika ya 15 baada ya kushindwa kuitendea haki pasi  Mohamed Rashidi.

Dakika 26 AFC Leopars walipata majanga baada ya kipa wao Adira kuumia na nafasi kuchukuliwa na Ezekiel Owade ambapo walijibu mashambulizi ya Simba  Eugene Mokangola  kupiga shuti lililotoka nje sentimeta chache.

Leopard waliendelea kujenga mashambulizi ya kutaka kusawazisha bao hilo kupitia kwa  Brian Marita na Christopher Oruchu lakini  wakakwama kutokana na uimara wa safu ya ulinzi ya Simba.

Zikiwa zimesalia dakika 5 kabla ya mapumziko Mohamed Ibrahim akaachia shuti ukiwa ni mpira adhabu na kuiandikia Simba bao pili lakini Leopard nao wakapa bao la kwanza kupitia kwa Mokangola ikiwa ni krosi ya Baker Lukoya.

Hadi mapumziko Simba ikachomoka uwanjani ikiongoza kwa idadi ya mabao 2-1.Kipindi cha pili kilianza kwa kasi lakini alikuwa Bocco tena aliyeiandikia Simba bao la tatu akiunganisha krosi ya  Mohamed Ibrahim kabla Marcel Kaheza kufunga la nne.

Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu kwa Leopard kutaka kusawazisha huku Simba ikijaribu kuongeza lakini wageni hao ndio waliomaliza mchezo kwa kupata bao la pili na kufanya mchezo huo kumalizika kwa Wekundi wa Msimbazi kuibuka na ushindi wa mabao 4-2.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here