Home Michezo kitaifa SIMBA HII SASA SIFA

SIMBA HII SASA SIFA

726
0
SHARE

SAADA SALIM NA MAREGES NYAMAKA,

WENYE nafasi yao wamerejea. Tena wamerejea kwa kishindo cha haja kwa kutembeza ‘kipigo cha sifa’ cha mabao 3-0 dhidi ya Prisons ya Mbeya na kurejea tena kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Wekundu hao wa Msimbazi licha ya kwamba waliibuka na ushindi huo, lakini pia walicheza kandanda la kuvutia huku straika wao Mrundi, Laudit Mavugo, ambaye awali alionekana kusuasua, akionyesha uhai mkubwa.

Waliowatoa uwanjani mashabiki wa Simba kwa shangwe ni Juma Luizio, aliyefunga bao la kwanza, Ibrahim Ajib, aliyefunga bao la pili pamoja na Mavugo aliyefunga bao la tatu na la ushindi.

Wekundu hao wa Msimbazi walianza kupata bao la kwanza katika dakika ya 18 likifungwa na Luizio, akiunganisha mpira wa kichwa uliopigwa na Novaty Lufunga ambaye alikuwa kwenye harakati za kuunganisha krosi ya Javier Bokungu aliyoichonga kutoka winga ya kulia.

Wakati Prisons wakijiuliza wamefungwaje bao hilo moja, walijikuta wakipachikwa bao la pili lililofungwa kwa ustadi mkubwa na Ajib akiunganisha vizuri pasi safi iliyopigwa na Mrundi, Mavugo.

Mabao hayo yaliwafanya Prisons kuanza kuzinduka wakitaka kusawazisha lakini walijikuta wakienda mapumziko wakiwa nyuma kwa mabao hayo 2-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa Prisons kulisakama lango la Simba wakitaka kusawazisha lakini uimara wa safu ya ulinzi ya wekundu hao wa Msimbazi iliyokuwa chini ya Method Mwanjali ilikaa imara.

Baada ya kuona Prisons wanakuja juu, Simba walitulia na kuanza kupanga mashambulizi na kufanikiwa kupata bao la tatu likifungwa kwa kichwa na Mavugo katika dakika ya 68, akiunganisha krosi iliyochongwa kutoka winga ya kushoto na Ajib.

Nusura Simba wapate bao la nne katika dakika ya 73 kupitia kwa Mwinyi Kazimoto aliyechukua nafasi ya Mwanjali aliyetoka ambapo shuti lake lililotokana na pasi ya Mavugo lilidakwa vizuri na kipa.

Simba walizidi kulishambulia lango la wapinzani wao hao ambapo dakika ya 80, Shiza Kichuya, aliyeingia kuchukua nafasi ya Ajib, aliachia shuti kali lililogonga mwamba wa juu na kurudi uwanjani na mabeki kuokoa.

Matokeo hayo yanaifanya Simba kukaa kileleni wakifikisha pointi 51 katika michezo 22 waliyokwisha kucheza na sasa wakienda kujipanga kwa ajili ya mchezo wao dhidi ya Yanga Februari 25, mwaka huu Uwanja wa Taifa.

Katika mchezo huo Simba iliwakilishwa na Daniel Agyei, Janvier Bokungu, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Novaty Lufunga, Method Mwanjali/Mwinyi Kazimoto, James Kotei, Said Ndemla, Muzamir Yassin, Laudit Mavugo, Ibrahim Ajib/Pastory Athanas na Juma Luizio/Shiza Kichuya.

Prisons iliwakilishwa na Laurian Mpalile, Aaron Kalambo, Salum Kimenya, James Mwasote, Nurdin Chona, Jumanne Elfadhil, Lambert Sibiyanka, Kazungu Nchinjayi/Kassim Hamisi, Victor Hangaya/Salum Bosco, Mohammed Samatta na Benjamin Asukile/Meshack Suleiman.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here