Home Habari Simba inachapa tu

Simba inachapa tu

455
0
SHARE

NA REBECCA LUZUNYA, SHINYANGA

AMA kweli Simba wamedhamiria kutwaa ubingwa msimu huu, ndiyo maana inachapa tu kila timu inayokutana nayo na jana iliwabamiza Mwadui FC mabao 3-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, uliochezwa kwenye Uwanja wa Kambarage, mkoani Shinyanga.

Waliopeleka kilio kwa Mwadui FC ni Shiza Kichuya, aliyefunga bao moja huku Mohamed Ibrahim, maarufu kama ‘Mo’ akifunga mawili na kuwafanya Wekundu hao wa Msimbazi kuzidi kujichimbia kileleni.

Mchezo ulianza kwa kasi, huku timu zote mbili zikisomana ambapo kila moja alianza kwa mashambulizi ya kushtukiza na kadri dakika zilivyokuwa zinakwenda ndivyo mchezo ulivyokuwa ukiongezeka kasi.

Simba ndio wa kwanza kufika langoni mwa wapinzani wao hao ambapo katika dakika ya tano, Laudit Mavugo aliwachambua mabeki wa Mwadui na kuachia mkwaju ambao ulipaa juu, huku akishindwa tena kutumia nafasi kama hiyo dakika ya saba.

Baada ya kuona Simba wanakuja juu, Mwadui walianza kutulia na kupanga mashambulizi ambapo katika dakika ya 14, Rashid Ismail aliachia shuti kali lililopaa juu mwa lango la Wekundu hao wa Msimbazi, huku dakika ya 25 Kichuya akishindwa kuunganisha kwa kichwa krosi ya Mavugo na mpira kupaa juu.

Baada ya kuona muda unakwenda Simba walitulia na kupanga mashambulizi na kufanikiwa kupata bao safi dakika ya 32, likifungwa na Mohamed Ibrahim, kutokana na pasi iliyopigwa na Mavugo kutoka winga ya kushoto.

Bao hilo liliwashtua Mwadui, ambao walianza kulinyemelea lango la Simba, ambapo katika dakika ya 34 nusura wajipatie bao, baada ya kipa Vincent Angban kutaka kudaka mpira ukaruka juu na kumgonga kwenye pasi la uso na kuokolewa na Method Mwanjale.

Katika dakika ya 35 Mzamiru Yassin alikosa nafasi ya wazi ya kuipatia Simba bao la pili, baada ya kushindwa kuunganisha pasi ya Mwinyi Kazimoto, ambapo lango lilikuwa wazi akataka kupiga na mpira ukampita kirahisi.

Simba walijiandikia bao la pili katika dakika ya 45 kupitia kwa Shiza Ramadhan Kichuya, akiunganisha vizuri pasi ya Mohamed Ibrahim, aliyoipiga kutoka winga ya kulia na kuzifanya timu hizo kwenda mapumziko Wekundu hao wa Msimbazi wakiwa mbele kwa mabao hayo mawili.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kubwa, Mwadui wakitaka kusawazisha, huku washambuliaji wao wakiongozwa na Paul Nonga, wakifanya kazi kubwa, lakini ukuta wa Simba uliokuwa chini ya Jjuuko Murushud, ulisimama imara.

Wekundu hao wa Msimbazi walijipatia bao la tatu katika dakika ya 50 kipindi cha pili kupitia kwa Mo Ibrahim, kutokana na pasi safi kutoka kwa Ame Ally, aliyeingia kuchukua nafasi ya Mavugo.

Katika dakika ya 70 Mwadui walifanya shambulizi zuri, lakini shuti la Paul Nonga lilishindwa kulenga na kujaribu tena dakika ya 79 na shuti kushindwa tena kulenga goli.

Katika dakika ya 80 Mzamiru Yassin alishindwa kuunganisha mpira kwa kichwa kutokana na krosi ya Ame Ally, ambapo hadi dakika 90 zinamalizika Wekundu hao wa Msimbazi waliibuka na ushindi huo wa mabao 3-0.

Kutokana na ushindi huo, Wekundu hao wa Msimbazi wamezidi kujichimbia kileleni, wakiwa na pointi 32, huku Shiza Kichuya naye akizidi kuwakimbia akina Amis Tambwe wa Yanga kwenye mbio za ufungaji, baada ya kufikisha mabao nane.

Katika mchezo huo, Mwadui FC ambao walikuwa wenyeji waliwakilishwa na Shabani Hassan ‘Kado’, Iddy Mobby, David Luhende, Shaaban Aboma, Joram Mgeveke, Abdallah Mfuko, Salim Khamis, Morris Kaniki, Paul Nonga, Rashid Ismail na Miraji Adam.

Simba iliwakilishwa na Vicent Angban, Janvier Bukungu, Mohamed Zimbwe, Method Mwanjale, Jjuuko Murshid, Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Mwinyi Kazimoto/Said Ndemla, Laudit Mavugo/Ame Alli, Shiza Kichuya/Ibrahim Ajib, Mohamed Ibrahim.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here