SHARE

NA MAREGES NYAMAKA

MNYAMA hataki kulaza damu, baada ya ligi kusimama kwa muda ili kupisha mechi ya timu ya taifa ‘Taifa Stars’ mwishoni mwa wiki hii, Simba wameona isiwe shida wachezaji wakae tu muda wote ambapo wanatarajia kucheza mechi moja ya kirafiki kesho.

Simba walifanikiwa kuanza ligi kwa kishindo mwishoni wa wiki kwa kuibuka na ushindi mnono wa mabao 7-0 mbele ya maafande wa Ruvu Shooting ya mkoani Pwani.

Kocha wa kikosi hicho, Joseph Omog, aliliambia DIMBA Jumatano kuwa watacheza mchezo huo wa kirafiki ili kuendelea kuwaweka wachezaji wake katika utimamu wa mwili muda wote (match-fitness).

“Tunaendelea na mazoezi yetu kila siku asubuhi lakini hiyo haitoshi, kwani tunatarajia kucheza mchezo wetu wa kirafiki Alhamisi dhidi ya Hard Rock ya Pemba, ili miili ya wachezaji iendelee kuwa fiti, ambapo Septemba 3 tunaingia kambini rasmi kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Azam FC,” alisema.

Wekundu hao wa Msimbazi wanatarajia kushuka dimbani Septemba 6 kuendelea kusaka pointi dhidi ya Azam, mtanange utakaopigwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here