Home Habari Simba mwendo wa hesabu

Simba mwendo wa hesabu

328
0
SHARE

KIZAANA EZEKIEL TENDWA


UNAUKUMBUKA msemo usemao ‘adui yako muombee njaa?’ Hiki ndicho Simba inakifanya sasa kwa kuziombea mabaya Yanga na Azam FC mechi zao za viporo vya Ligi Kuu ‘zichache’ ili wasitibue mbio zao za kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu.
Yanga na Azam FC zitakuwa na mechi za Ligi Kuu wikiendi hii, zikijaribu nazo kuweka hesabu zao za ubingwa vyema, lakini kwa Simba ambayo haitakuwa na mchezo wowote, inachokifanya ni kuziombea dua mbaya timu hizo zipoteze mechi hizo za viporo.
Ikumbukwe Simba ndiyo vinara wa Ligi hiyo, wakiwa wamecheza mechi 24 na kuweka kibindoni pointi 57, wakifuatiwa na Yanga iliyocheza mechi 21, wakiwa na pointi 50 sawa na Azam yenye idadi kama hiyo ya mechi na pointi.
Kimahesabu iwapo Yanga na Azam zitashinda kila mmoja mechi zake zote zilizosalia, wataipiku Simba kwa pointi mbili, hivyo kufanya ubingwa kuamuliwa na timu hizo kwa idadi ya mabao kufunga na kufungwa.
Kwa kuzingatia muktadha huo, Simba hesabu zake sasa ni kutaka kushinda mechi zake zote na kuomba dua wapinzani wake hao wateleze kwenye mbio hizo na kutwaa ubingwa kilaini baada ya kuusotea kwa misimu mitatu bila mafanikio.
Katika michezo hiyo ya mwishoni mwa wiki hii, Yanga watakuwa Uwanja wa Taifa kuwakabili Kagera Sugar, huku Azam FC wakiwa wageni wa Toto African ya jijini Mwanza Uwanja wa CCM Kirumba.
Endapo timu hizo zitapata matokeo ya sare au kupoteza, inamaanisha kuwa hesabu za Simba zitakwenda sawa na ikitokea tena wakapata matokeo mengine yasiyoridhisha katika viporo vingine vilivyobakia, itakuwa kicheko kikubwa kwa Wekundu hao wa Msimbazi.
Hali halisi iko hivi, kama Yanga na Azam watashinda viporo vyao vilivyobakia watafikisha jumla ya pointi 59 ambapo watawapita Simba kwa pointi mbili, lakini katika viporo hivyo kama itatokea sare moja tu ina maana watalingana pointi na Wekundu hao wa Msimbazi.
Kama Yanga na Azam kila moja itapoteza kiporo kimoja na kushinda viwili watafikisha pointi 56 na kuwaacha Wekundu hao wa Msimbazi kutamba kileleni na kuusaka ubingwa kwa nguvu, lakini pia kama timu hizo zitapata sare katika viporo hivyo vyote vitatu, hakuna shaka njia itakuwa nyeupe kwa Simba.
Kama hali itakuwa hivyo na Simba wakafanikiwa kushinda michezo yao sita iliyobakia, watakuwa wametwaa ubingwa huo na kuweka historia nzuri ya kumaliza Ligi wakiwa na pointi nyingi katika misimu ya hivi karibuni.
Unajua ikoje? Kwa sasa Simba wanazo pointi 57 kibindoni na kama watafanikiwa kushinda michezo yao sita iliyobakia ambayo ni sawa na pointi 18, watakuwa wamejikusanyia jumla ya pointi 75 na kuweka historia nyingine ya kukumbukwa.
Katika misimu ya hivi karibuni hakuna timu iliyofanikiwa kufikia rekodi hiyo ambapo msimu uliopita Yanga walimaliza Ligi kama mabingwa, wakiwa na jumla ya pointi 55 ambazo mpaka sasa zimeshapitwa na Simba, wakati huo timu zilikuwa 14.
Katika msimu wa 2013/14, wakati huo pia timu shiriki zikiwa 14, Azam FC ambao walitwaa ubingwa huo walimaliza wakiwa na pointi 62, ambazo Simba wakishinda michezo yao miwili tu kati ya sita iliyobakia watazipita.
Msimu mwingine wa 2012/13, wakati huo Yanga wakitwaa ubingwa, walimaliza Ligi wakiwa na jumla ya pointi 60, ambazo Simba wakishinda mchezo wao mmoja tu kati ya sita iliyobakia watazikuta.
Kutokana na hali hiyo, ndiyo maana Wekundu hao wa Msimbazi wamesisitiza kutokuingiza timu uwanjani hadi pale Yanga na Azam watakapomaliza viporo vyao, hasa wakati huu Ligi inapoelekea ukingoni.
Wekundu hao wa Msimbazi wana misimu mitatu mfululizo bila kuonja ladha ya ubingwa na sasa wamesema watafanya kila linalowezekana ili kupata ubingwa msimu huu na kuepuka kejeli kutoka kwa wapinzani wao wa jadi, Yanga, kwamba ni ‘Wamchangani’.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here