Home Habari Simba sasa ni mwendo wa magari

Simba sasa ni mwendo wa magari

1134
0
SHARE

NA EZEKIEL TENDWA

UKISIKIA jeuri ya fedha ndiyo hii. Baada ya Simba kuteswa kwa misimu kadhaa na Yanga hasa kutokana na kukosa fedha za kutosha kujiendesha, sasa uongozi wa klabu hiyo umeamua kufanya kweli kwa kutoa motisha nono kwa wachezaji wao.

Katika misimu minne iliyopita ambayo wameukosa ubingwa, haikuwa ajabu kuzagaa tetesi za wachezaji wa Simba kucheleweshewa mishahara yao, hali iliyokuwa ikitajwa kama inashusha morali lakini sasa mambo yamebadilika.

Msimu huu Simba wameingia kivingine kabisa huku matajiri wa timu hiyo ambao misimu iliyopita walikuwa pembeni, wote wamerudi na wamekuwa kitu kimoja huku wakishirikiana kuwapa wachezaji kila wanachokihitaji.

Moja ya vitu ambavyo vinawapa morali wachezaji ni kuwa na uhakika wa mishahara yao hasa baada ya mfanyabiashara na tajiri namba moja nchini, Mohamed Dewji ‘Mo’, kujitwisha jukumu la kulipa mishahara yao katika kipindi hiki ambacho wanaelekea kwenye mabadiliko ya hisa.

Wekundu hao wa Msimbazi kwa sasa wapo kwenye mchakato wa kubadili mfumo na kuingia kwenye ule wa hisa ambao Mo ameweka mezani kitita cha Sh bilioni 20 za Kitanzania ambapo katika kipindi hiki ambacho mchakato huo ukiendelea, mfanyabiashara huyo ameamua kulipa mishahara ya wachezaji.

Mbali na hilo, pia Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hanspope, amekuwa akijitolea kuwapa magari wachezaji ambao wamekuwa wakionyesha juhudi kubwa ndani ya uwanja.

Pope anatoa zawadi hizo kama mwanachama mwenye mapenzi mema na klabu hiyo ambapo alianza kufanya hivyo kwa beki wa kushoto, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ huku Shiza Kichuya naye akipata zawadi hiyo kutokana na kazi nzuri anayoifanya hususani pale alipofanikiwa kufunga bao la kusawazisha dhidi ya Yanga Jumamosi iliyopita.

Kwa sasa wachezaji ambao muda wowote wanaweza kulamba zawadi hiyo ya gari kutokana na kazi nzuri wanayoifanya ni Ibrahim Ajib, Jonas Mkude, Muzamiru Yassin pamoja na Jjuuko Murushid ambaye licha ya kwamba mara kadhaa anatokea benchi lakini kazi yake inaonekana.

Simba wameuanza msimu huu kwa kishindo wakiwa hawajapoteza mchezo wowote katika michezo saba waliyokwisha kucheza mpaka sasa wakiwa kileleni na pointi zao 17.

Mafanikio ambayo Simba wanayapata kwa sasa yanatajwa kwamba ni kutokana na umoja walionao tofauti na msimu uliopita timu ilivyokuwa na makundi likiwamo lile lililopachikwa jina la ‘Simba Ukawa’.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here