Home Habari SIMBA SC YATOA ZAWADI YA X-MASS

SIMBA SC YATOA ZAWADI YA X-MASS

496
0
SHARE

NA SAADA SALIM,

SIMBA imetoa zawadi ya Krismasi kwa mashabiki wake baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya maafande wa JKT Ruvu mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kuzidi kujikita kileleni mwa msimamo.

Bao hilo pekee la ushindi lilifungwa na kiungo mshambuliaji, Mzamiru Yasin, katika dakika ya 45 ya kipindi cha kwanza akiunganisha kwa kichwa krosi iliyochongwa na Pastory Athanas kutoka winga ya kulia ambapo mpaka timu hizo zinakwenda mapumziko Wekundu hao wa Msimbazi walikuwa mbele kwa bao hilo 1-0.

Kabla ya bao hilo timu zilikuwa zikishambuliana kwa zamu ambapo washambuliaji wa pande zote walikuwa wakitafuta namna ya kupenya ngome za wapinzani wao, hali iliyoufanya mchezo huo kuwa mkali na wa kusisimua.

Mshambuliaji wa Simba, Pastory Athanas, ambaye alisajiliwa katika dirisha dogo la usajili kutoka Stand United, alionyesha uwezo mkubwa na kama si juhudi za mabeki wa JKT Ruvu kusimama imara huenda kipindi hicho cha kwanza Wekundu hao wa Msimbazi wangekwenda mapumziko wakiongoza kwa mabao zaidi ya moja.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku JKT Ruvu wakitaka kusawazisha na Simba wakitaka kuongeza bao lingine hali iliyoufanya mchezo kuzidi kuchangamka.

Katika dakika ya 55, Athanas aliachia shuti kali akiwa nje ya eneo la hatari na kipa wa JKT Ruvu kuokoa kwa kuutema lakini akauwahi na kuudaka kabla washambuliaji wa Wekundu hao wa Msimbazi hawajauwahi na kuleta madhara.

Atupele Green ambaye aliingia kuchukua nafasi ya Salim Gilla, aliongeza uhai kwenye safu ya ushambuliaji ya JKT Ruvu lakini mabeki wa Simba waliokuwa chini ya Method Mwanjali na Abdi Banda, ilikaa vizuri na kuokoa hatari zote.

Kadiri muda ulivyozidi kwenda ndivyo ambavyo mpira ulivyozidi kuwa mkali lakini hadi dakika 90 zinamalizika Simba waliibuka na ushindi wa bao 1-0 na kuzidi kujikita kileleni wakifikisha jumla ya pointi 41.

Katika msimamo huo wa ligi, Yanga ndio wanaofuatia wakiwa na pointi 37 hasa baada ya kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na African Lyon, mchezo uliochezwa juzi Ijumaa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo huo Simba iliwakilishwa na Daniel Agyei, Javier Bukungu/Hamad Juma, Mohamed Hussein, Abdi Banda, Method Mwanjali, James Kotei/Said Ndemla, Muzamiru Yassin, Shiza Kichuya, Jonas Mkude pamoja na Pastory Athanas.

Kwa upande wao JKT Ruvu ambao walikuwa wenyeji waliwakilishwa na Hamis Seif, Salim Gilla, Michael Aidan, Frank Nchimbi, Yusuph Chuma, Kelvin Nashon, Edward Joseph, Hassan Dilunga, Hassan Materema, Musa Juma pamoja na Ally Bilaly.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here