SHARE
 Mo aongoza jahazi kutafuta ushindi ndani na nje

NA SAADA SALIM

VIGOGO wa Simba, wakiongozwa na bilionea wao, Mohamed Dewji ‘Mo’, wanajua kuwa Jumamosi ya wiki hii kikosi chao kinakabiliwa na mchezo mgumu wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo, na sasa wameamua kujifungia kuweka mambo sawa.

Simba, ambao wametinga hatua hiyo baada ya kuziangusha timu  vigogo, zikiwamo Al Ahly ya Misri na AS Vita ya DR Congo, watacheza dhidi ya TP Mazembe Jumamosi Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Baada ya mchezo huo, Simba watasafiri kwenda DR Congo kwa ajili ya mchezo wa marudiano unaotarajiwa kuchezwa Aprili 13, mwaka huu na timu itakayopata matokeo mazuri ya jumla itatinga nusu fainali.

Licha ya kwamba Simba walifungwa ugenini na Ahly na Vita, waliwekamipango madhubuti iliyowafanya kutinga hatua ya robo fainali na sasawanaisubiri kwa hamu TP Mazembe.

Mipango hiyo ndiyo iliyowafanya kuwafunga JS Saoura ya Algeria mabao 3-0, ikawafunga Ahly bao 1-0 nabaadaye kuwaangamiza kabisa Vita
mabao 2-1 na kutinga hatua ya robo fainali, hali iliyozishtua timu nyingi vigogo barani Afrika.
Akizungumza na DIMBA Jumatano, Katibu wa klabu hiyo, Anold Kashembe, alisema viongozi wa sekretarieti walikutana juzi kujadili namna timu yao itakavyopambana na kupata ushindi katika mechi za nyumbani na ugenini, ikizingatiwa kuwa hatua hii ni ya mtoano.

“Lazima tuwe na mikakati, maana mchezo huo ni mgumu, hata michezo iliyopita tulifanya vikao vizito ambavyo nadhani vilichangia kupata matokeo mazuri na ndicho tunachokifanya kwa sasa.

“Haiwezekani timu inacheza mchezo mkubwa namna hiyo halafu viongozi tuwe tumelala tu, niwahakikishie mashabiki kwamba tupo imara navikao vinaendelea kama kawaida yetu,” alisema.

Alisema uongozi wa juu umeshakutana na benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu Patrick Aussems na kuweka mikakati yao na pia wanaendeleakushirikiana kuona namna ya kupata matokeo mazuri.

Alisema mikakati ilianza tangu walipomaliza mchezo wao dhidi ya Mbao FC, uliochezwa Uwanja wa Jamhuri, mkoani Morogoro na kushinda mabao 3-0, ambapo walikaa na wachezaji na kuzungumza nao kwa kirefu.

Kwa upande wake Aussems, ameliambia DIMBA Jumatano kuwa, vijanawake watapambana kama walivyofanya dhidi ya Ahly na AS Vita, lakinimara hii hawatakubali timu iruhusu kufungwa ugenini.

“Baadhi ya mashabiki wanadhani tulivyofungwa mabao mengi ugenini dhidi ya Al Ahly na AS Vita itakuwa hivyohivyo dhidi ya TP Mazembe, nipende kuwaambia tumejipanga vizuri nyumbani na ugenini.

“Hatuwezi kukubali tena kufungwa idadi kama ile, kilichopo ni kupataushindi mnono nyumbani ili tukifika ugenini kama hatutashinda angalau tupate sare, hiyo ndiyo mikakati yetu,” alisema.

Simba walianza michuano hiyo kwa kuwafunga Mbabane Swallows ya Eswatini jumla ya mabao 8-1 hatua ya awali, wakianza kushinda mabao 4-1 nyumbani na kushinda 4-0 ugenini.  

Baadaye wakakutana na Nkana FC ya Zambia na kufungwa mabao 2-1 ugenini, kabla ya kushinda mabao 3-1 nyumbani na kutinga hatua ya makundi kwa ushindi wa jumla ya mabao 4-3.

Hatua hiyo ya makundi walikuwa kundi D lililokuwa na Ahly, Vita pamoja na Saoura na Wekundu hao wa Msimbazi wakashika nafasi ya pili, wakijikusanyia pointi tisa, huku Ahly wakishika usukani kwa pointi 10.

Michezo yao yote ya nyumbani walishinda huku wakifungwa michezo yao yote ya ugenini, hatua hiyo ya makundi wakishinda mabao 3-0 dhidiya Saoura, wakashinda bao 1-0 dhidi ya Ahly na 2-1 dhidi ya Vita hukuwakifungwa ugenini mabao 5-0 na Ahly na kipigo kama hicho dhidi ya Vita na kufungwa mabao 2-0 na Saoura.

Katika hatua nyingine, Simba kupitia mkuu wao wa Idara ya Habari na
Mawasiliano, Hajji Manara, alitaja viingilio vya mchezo huo dhidi ya Mazembe kuwa ni Sh 4,000 kwa mzunguko , VIP B Sh 10,000, VIP A Sh 20,000 na Platinum Sh 100,000.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here