Home Habari SIMBA WAMPIGIA HESABU PLUIJM

SIMBA WAMPIGIA HESABU PLUIJM

1943
0
SHARE
NA EZEKIEL TENDWA

SIMBA wameshatua jijini Dar es Salaam wakitokea Zanzibar, baada ya kutupwa nje ya michuano ya Kombe la Mapinduzi, lakini wamerejea wakiwa na jina mkononi la Kocha Mkuu wa Singida United, Hans Van de Pluijm, kwamba Mholanzi huyo anafaa kuvaa viatu vya Joseph Omog.

Simba bado wanahangaika kumpata kocha mkuu, baada ya kumtema Omog na sasa jina la Pluijm linatajwa sana kwamba akitua kwa Wekundu hao wa Msimbazi, bila shaka kikosi chao ambacho kimesheheni wachezaji wa viwango vya juu, kitatisha ndani na nje ya nchi.

Wekundu hao wa Msimbazi wanakumbuka jinsi Pluijm alivyoipika Yanga ikawa inacheza soka la kisasa kabla ya kutimkia Singida United, ambayo nayo imekuwa tishio kwa kila timu, ndiyo maana wanapiga hesabu za kumnyakua kabla michuano ya kimataifa haijaanza.

Simba wanashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, wakianza nyumbani dhidi ya Gendarmerie Tnale ya nchini Djibout na sasa wanapambana kuhakikisha wanampata kocha mkuu mapema iwezekanavyo, huku jina la Pluijm likiwa gumzo kwamba huenda akapewa jukumu la kuiongoza timu hiyo.

Kigogo mmoja wa Simba ameliambia DIMBA Jumatano kwamba, Pluijm ni mmoja wa makocha wenye uwezo mkubwa na kwamba wanaangalia uwezekano wa kuzungumza naye, kwani kazi aliyoifanya akiwa Yanga na sasa Singida United, inaonyesha wazi ni mpambanaji.

“Kama unavyojua kwa sasa (Simba) tunatafuta kocha mkuu mwenye uwezo mkubwa, ikizingatiwa kuwa tunausaka ubingwa wa ligi kuu kwa kila hali lakini pia tunakabiliwa na michuano migumu ya Kombe la Shirikisho Afrika.

“Ni ukweli ulio wazi kwamba Pluijm ni mmoja wa makocha wanaoheshimika na sisi tunatamani kuwa naye kwenye kikosi chetu hasa wakati huu, ngoja tuone itakavyokuwa lakini ukweli ni kwamba tunamtaka sana,” alisema kigogo huyo.

Mbali na kigogo huyo, hata kwenye ‘magrupu’ ya mitandao ya kijamii, mashabiki wa Simba wamekuwa wakiutaka uongozi wao kufanya kila linalowezekana kuhakikisha wanamchukua kocha huyo wakiamini kwamba anaweza akawarudishia heshima yao iliyopotea kwa misimu mitano mfululizo.

Baada ya taarifa hizo kuvuja kwamba Simba wanampigia hesabu Pluijm, DIMBA Jumatano lilikwenda mbali zaidi na kumtafuta kocha huyo ambaye leo atakiongoza kikosi chake kucheza mchezo wa nusu fainali wa michuano ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Azam FC, ili mwenyewe atoe kauli.

Mholanzi huyo alisema kwa sasa hawezi kuzungumza lolote kwani bado anao mkataba na Singida United na kwamba anashukuru kuona kazi yake inakubalika na kila mtu.

“Siwezi kusema kitu chochote kuhusu jambo hilo, bado niko chini ya mkataba na Singida United, niseme tu nashukuru kwani kama unafanya kazi na watu wanaikubali ni jambo jema,” alisema.

Wadau wa soka wanaamini kwamba kama viongozi wa Simba watapambana na kufanikisha zoezi hilo, watakuwa wamelamba dume kwani Pluim ni mmoja wa makocha wenye weledi mkubwa na pia huwa anaishi vizuri na wachezaji kama baba.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here