SHARE

SAADA SALIM NA CLARA ALPHONCE,

SIMBA jana wamechekelea baada ya kusikia Yanga kafungwa na Mbao FC bao 1-0, sasa akili na masikio yao wanaelekeza FIFA, wakisubiri majibu ya rufaa yao waliyoiwasilisha kudai pointi tatu za Kagera Sugar.

Hiyo inafuatia Simba kuibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Mwadui FC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, huku Yanga wakipoteza mechi yao hiyo kwa kuchapwa bao hilo 1-0 na Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Simba imepeleka malalamiko Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo (CAS) mjini Zurich, Uswisi kudai pointi tatu za chee walizopokonywa, baada ya kupewa kimakosa kufuatia kufungwa na Kagera Sugar.

Baada ya kufungwa 2-1 na Kagera Sugar Aprili 2, mwaka huu Uwanja wa Kaitaba, Simba walimkatia rufaa beki Mohammed Fakhi na wakapewa na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi pointi tatu, kabla ya Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji kuwapokonya pointi hizo kufuatia Kagera Sugar kukata rufaa pia.

Simba jana walirahisishiwa kazi na Mbao FC, walioifunga Yanga bao 1-0, na hivyo kufikisha pointi 36 zilizowabakisha Ligi Kuu.

Na sasa Wekundu wa Msimbazi wamefikisha pointi 68 sawa na Yanga, lakini mahasimu wao hao wakakabidhiwa kombe la ubingwa kutokana na wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Hivyo kama FIFA wakiwapa Simba pointi tatu, watakuwa wamefikisha pointi 71 na hivyo kutawazwa mabingwa wapya wa msimu huu.

Hivi karibuni Makamu wa Rais wa klabu hiyo, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, alithibitisha kupeleka malalamiko hayo kwa mahakama ya CAS iliyo chini ya FIFA na kwa sasa wanasubiri majibu kutoka katika shirikisho hilo.

Hata hivyo, kanuni za ligi kuu zinaeleza wazi kuwa, mchezaji akichezeshwa wakati ana kadi tatu za njano basi timu hiyo inapokwa pointi tatu na mabao matatu.

Ili kuthibitisha bado wana imani na FIFA, wachezaji wa Simba jana waligoma kupokea zawadi ya mshindi wa pili pamoja na medali zao mpaka watakapoletewa majibu na FIFA.

Katika mchezo wa jana jijini Dar es Salaam, dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika Simba ikiwa inaongoza kwa mabao 2-1 Uwanja wa Taifa, mabao yake yakifungwa na winga Shiza Ramadhani Kichuya na mshambuliaji Ibrahim Ajib Migomba, huku la Mwadui likifungwa na Paul Nonga.

Kichuya alianza kufunga dakika ya 17 kwa mkwaju wa penalti, baada yeye mwenyewe kuchezewa rafu na kipa wa Mwadui, Shaaban Hassan Kado.

Na kabla Mwadui hawajakaa sawa, Ajib akawatandika bao la pili dakika ya 24, akimalizia pasi ya Juma Luzio. Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Nonga akaifungia Mwadui dakika ya 42, akimalizia krosi ya Hassan Kabunda.

Kikosi cha Simba SC jana kilikuwa: Agyei Daniel, Janvier Bukungu, Mohammed Hussein, James Kotei, Juuko Murshid, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Yassin Mzamiru, Laudity Mavugo/Mwinyi Kazimoto, Ibrahim Ajibu na Juma Luizio/Said Ndemla.

Mwadui: FC Shaaban Hassan, David Luhende, Nassor Hemed, Abdallah Mfuko, Joram Mgeveke, Razack Khalfan, Awadh Juma, Miraj Athumani, Salim Kabunda/Abdallah Seseme, Hassan Kabunda na Paul Nonga.

1 COMMENT

  1. Maoni:jamali malinzi na kabineti yake yote, ndiyo chanzo cha kufeli mpira wa amani Tanzania,timu zimewekeana uadui kuliko miaka ya zamani, waachie madalaka!

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here