Home Habari SIMBA YA MBELGIJI UNAGUSA UNAACHIA

SIMBA YA MBELGIJI UNAGUSA UNAACHIA

1849
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU


MAMBO ni motoo! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema, kwani lile soka la ‘kampa kampa tena’ limerudi rasmi tena Simba baada ya kocha wao, Mbelgiji Patrick Aussems, kuwaambia wachezaji wake anataka mpira wa kuvutia kama ilivyo kwa Barcelona ya Hispania.

Simba wamejichimbia nchini Uturuki wakiwa wamemaliza wiki sasa lakini unaambiwa kocha huyo tangu aanze kazi amekuwa akiwafundisha vijana wake pasi zile za kugusa na kuachia zoezi ambalo wachezaji walionekana kulimudu vilivyo.

Mbelgiji huyo leo ataangalia kazi aliyoifanya kama imeeleweka vizuri kwa wachezaji wake pale timu hiyo itakapocheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Mouloudia Club Oujda ya Morocco, ambayo nayo imeweka kambi nchini humo.

Licha ya kwamba msimu uliopita Simba walitwaa ubingwa, lakini mashabiki wengi walionekana kutovutiwa na aina ya ufundishaji wa kocha aliyepita, Pierre Lechantre, raia wa Ufaransa, kwani timu ilikuwa inazuia zaidi lakini sasa wanaweza kuanza kutabasamu kutokana na hicho kinachofanywa na kocha wao mpya.

Katika mazoezi ya kikosi hicho kilichoweka kambi kwenye Hoteli ya The Green Park Kartepe and SPA, jijini Instanbul, Mbelgiji huyo na wasaidizi wake walikuwa wakiwafundisha wachezaji mbinu mbalimbali lengo likiwa ni kuhakikisha wanatetea ubingwa wao msimu ujao.

Akizungumza na DIMBA Jumatano, kocha msaidizi wa Simba, Masoud Djuma, alisema wachezaji wake wote wanaonyesha uwezo na kujituma hiyo ikimaanisha mazoezi hayo yanawasaidia sana.

“Tunaendelea vizuri, kila mchezaji anatakiwa apambane na kujituma na hivyo ndivyo ilivyo, kwa ujumla mambo yanavyoendelea yanafurahisha sana.

“Tutakuwa na mchezo wa kirafiki ambao nadhani utatupa sisi benchi la ufundi mwanga wa wapi pako vizuri na wapi tuparekebishe, yote kwa yote tupo kamili kwa msimu ujao,” alisema.

Mchezo huo dhidi ya Waarabau hao, unaweza kutoa taswira ya kikosi cha kwanza huku wengi wanasubiri kuona kombinesheni ya mastraika watatu John Bocco, Emmanuel Okwi pamoja na Meddie Kagere.

Kagere ameliambia DIMBA Jumatano kuwa, amepata muda mzuri wa kucheza na wenzake na amepewa ushirikiano wa kutosha huku akiahidi kwamba yupo tayari kwa mapambano.

“Napata ushirikiano mzuri kutoka kwa wenzangu, mashabiki wetu watarajie makubwa, mimi nimekuja Simba kucheza na nimekutana na wachezaji wenye uwezo mkubwa ndiyo maana nasema mashabiki watafurahi wenyewe,” alisema Kagere.

Katika uteuzi wa kupata kikosi cha kwanza, kocha Aussems atakuwa na kazi ya ziada kwenye safu ya ushambuliaji ambapo mbali na akina Okwi, Bocco na Kagere, wapo pia Mohammed Rashid na Adam Salamba.

Simba wanatarajia kurejea nchini Agosti 5 mwaka huu kwa ajili ya tamasha lao la ‘Simba Day’, linalotarajiwa kufanyika Agosti 8, mwaka huu watakapocheza na AFC Leopards ya Kenya iliyoalikwa kunogesha sherehe hizo katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here