SHARE

NA AYOUB HINJO


Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, wamelazimishwa suluhu ya 0-0 dhidi ya Ndanda FC, katika mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa jana Uwanja wa Nangwanda Sijaona, mjini Mtwara.

Tangu Ndanda FC ipande daraja haijawahi kuisumbua Simba popote timu hizo zilipokutana na hii ni mara ya kwanza kwa Wekundu hao wa Msimbazi kulazimishwa sare na hivyo kuacha rekodi katika mkoa huo.

Tangu Ndanda waanze kucheza Ligi Kuu msimu wa 2014/15, walijikuta wakiambulia vipigo mfululizo, lakini msimu huu wamejitutumua na kulazimisha suluhu hiyo ya 0-0.

Suluhu hiyo ni kama rekodi mpya kwa Simba, ambao wamekutana na Ndanda mara nne katika Uwanja huo na michezo yote Wekundu hao wa Msimbazi wakishinda.

Msimu wa 2014/15, Simba walipokutana na Ndanda Uwanja huo walishinda mabao 2-0, mchezo wa mzunguko wa pili, huku pia wakishinda bao 1-0 msimu wa 2015/16, mchezo pia wa mzunguko wa pili kabla ya msimu uliopita kushinda tena mabao 2-0.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, alisema vijana wake walipambana ili kupata matokeo mazuri, lakini ikashindikana, hivyo aliahidi kufanya vizuri michezo inayofuata.

“Hata hii pointi moja tuliyoipata tunashukuru, kwani wenzetu nao walicheza vizuri, kwa ujumla vijana wangu walijitahidi ili tushinde, lakini ikashindikana.

“Bado safari ni ndefu, kwani michezo ipo mingi, hivyo niseme kwamba tutapambana ili kuhakikisha tunatetea ubingwa wetu, licha ya kuwa kila timu imejipanga vizuri,” alisema.

Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Ndanda FC, Malale Hamsini, alisema vijana wake wametekeleza kile alichowaahidi na wanashukuru, kwani awamu hii hawajafungwa, tofauti na misimu mingine.

“Simba ni timu kubwa, ndiyo maana misimu iliyopita tumekuwa tukipata tabu kila tunapokutana nao, nashukuru kwamba leo (jana), tumepambana na kupata sare hiyo, wachezaji wangu wametekeleza majukumu niliyowapa,” alisema.

Mpaka sasa Simba ndiyo timu pekee ambayo haijaruhusu bao lolote katika michezo mitatu waliyocheza, wakishinda bao 1-0 dhidi ya Prisons mchezo wa ufunguzi na kupata tena ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mbeya City na jana wakalazimishwa suluhu ya 0-0 dhidi ya Ndanda.

Katika michezo mingine ya ligi hiyo iliyochezwa jana, Timu ya Prisons ya Mbeya iligawana pointi na Ruvu Shooting baada ya kufungana mabao 2-2.

Kikosi cha Lipuli FC kutoka mjini Iringa kilitoka suluhu ya 0-0 na Mtibwa Sugar, wakati Mbao FC ikionja machungu ya kufungwa baada ya kuchapwa bao 1-0 na JKT Tanzania.

Watoto wa Kinondoni, KMC, waliambulia kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Singida United na Biashara Mara ikitoka suluhu 0-0 na jirani zao wa Kagera Sugar.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here