SHARE

NA SAADA SALIM,

SIMBA wameshindwa kuonyesha cheche zao kwenye michuano ya SportPesa Super Cup, baada ya kufungwa na Nakuru All Stars jumla ya mabao 5-4 kwa njia ya penalti, baada ya kumaliza dakika 90 timu hizo zikiwa suluhu ya 0-0.

Aliyezamisha jahazi la Simba ni kipa wao, Daniel Agyei, ambaye alipiga penalti iliyoota mbawa, ikipaa juu, huku akishindwa kuokoa hata moja dhidi ya wapinzani wao hao.

Penalti za Simba zilifungwa na Javier Besala Bokungu, Mwinyi Kazimoto, Hafidh Mussa pamoja na beki mpya aliyetoka Rwanda, Fiston Munezero, huku Agyei akipaisha na kuifanya timu hiyo kushindwa kutinga hatua ya nusu fainali kama wenzao, Yanga.

Kwa upande wa Nakuru, penalti zao zilipigwa na Nturukundo Baraka, Aman Kiyata, Maina Kangethe, Amakanji Ekmba pamoja na Ngang’a Kamau.

Awali katika kipindi cha kwanza na cha pili, Simba walionekana kuelemewa na huenda ni kutokana na idadi kubwa ya wachezaji wao wa kikosi cha kwanza kukosekana kutokana na kambi ya timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ nchini Misri.

Katika mchezo huo, Simba iliwakilishwa na Daniel Agyei, Besala Bokungu, Mwambeleko Jamal, Feston Munezero, Mlipili Yusuph, Mwinyi Kazimoto, Masoud Bakari, Jamal Mnyate, Juma Luizio, Pastory Athanas, pamoja na Mohamed Ibrahim.

Nakuru wao waliwakilishwa na Lule Martin, Nganga Kamau, Wainaina Sadick, Mukhwana Sadicky, Amakanji Ekmba, Siwa Omondi, Amani Kyata, Ng’ang’a Anthony, Nandwa Sosi, Maina Kangethe pamoja na Kamau Ndungu.

Katika mchezo wa mapema uliozikutanisha Jang’ombe Boys dhidi ya Gor Mahia ya Kenya, mchezo huo ulishuhudia dakika 90 zikimalizika kwa Wakenya hao kutinga hatua ya nusu fainali baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Mabao ya Gor Mahia yalifungwa na Medie Kagere katika dakika ya 64, akiunganisha kwa kichwa krosi ya Muguna Kenneth, huku bao la pili likifungwa na Medie Kagere kwa njia ya penalti, katika dakika ya 83.

Timu zilizotinga hatua hiyo ya nusu fainali ni Yanga ambayo ndiyo pekee kutoka Tanzania, huku timu nyingine tatu zote zikitoka Kenya ambazo ni Gor Mahia, Nakuru All Stars pamoja na AFC Leopard.

Leo Jumatano Yanga itakipiga na AFC Leopards jioni, huku Gor Mahia ikikipiga na Nakuru All Stars.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here