SHARE

NA WINFRIDA MTOI

SIMBA hii haitishiki. Siku moja baada ya straika wao, John Bocco, kudaiwa kuwa amesaini mkataba na Polokwane City FC ya Afrika Kusini, uongozi wa klabu hiyo, umesema hakuna wakumng’oa mchezaji huyo Msimbazi.

Polokwane City FC waliibuka baada ya juzi kuona picha za Bocco akiwa anasaini mkataba mpya kukipiga Simba mbele ya mwekezaji wa klabu hiyo, mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘MO’.

Akizungumza na DIMBA jana, Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Klabu ya Simba, Crescentius Magori, alisema Bocco haendi popote na msimu ujao ataendelea kuitumikia timu hiyo.

Alisema baada ya kutokea mkanganyiko huo, walizungumza na uongozi wa klabu ya Polokwane FC ambao walikiri kufanya makosa ya kumsainisha mchezaji huyo, akiwa ndani ya mkataba.

Alisema kutokana suala hilo wamefikia makubaliano na hakuna mvutano wowote kati ya klabu hizo na kwamba wamekubali yaishe na Bocco ni mchezaji wa Simba.

“Hakuta utata wowote, Bocco ni mchezaji wa Simba, wale wamekubali kufanya makosa, kingine hakuna hela yoyote waliyomlipa mchezaji nakuwaje mchezaji wao?

“Mkataba wa Bocco na Simba ulikuwa unamalizika Juni, mwaka huu, haiwezekani kukamilisha usajili wa mchezaji ambaye bado hajamalizana na timu yake, kiufupi hilo limeisha Bocco ni mchezaji wetu hakuna mjadala.

“Ni sawa mchezaji anaruhusiwa kufanya mazungumzo na timu nyingine kama mkataba wake umebaki miezi sita lakini lazima klabu anayotoka itaarifiwe kwa barua kama TP Mazembe walivyofanya kwa Ajib,” alisema Magori.

CEO huyo aliwataka Wanasimba kutulia na kufahamu Bocco ni mchezaji halali wa Simba bila kutishwa na yale yanayoendelea katika mitandao.

Mshambuliaji wa Taifa Stars na nahodha wa Simba SC John Bocco amesaini mkataba mpya wa miaka miwili kuendelea kuichezea klabu hiyo.

Bocco ambaye alikuwa mchezaji bora wa Simba na Ligi Kuu msimu wa 2017/18 na amefungia timu hiyo mabao zaidi ya 30 Ligi kwa misimu miwili aliyoichezea timu hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here