SHARE

simbaNA MSHAMU NGOJWIKE

KITENDO cha Azam FC kuvutwa shati na Toto Africans ya Mwanza na kufanya mechi yake ya kiporo ‘kuchacha’, kimeifanya Simba kuzidi kuamka na kuanza kucheza na hesabu za mechi za Yanga.

Simba imechungulia ratiba na kugundua kuwa mahasimu wao Yanga wana wakati mgumu katika mzunguko huu wa pili kutokana na kuwa na mechi nyingi mikoani ambazo msimu huu wanaonekana kuwa na matokeo hasi kwao.

Kinachowapa kiburi Simba kwenye mbio zao za kutwaa ubingwa ni kuona wana asilimia kubwa ya ushindi kwani mechi nyingi zilizosalia kwao ni za nyumbani ambazo wanaweza kuzitumia vizuri.

Wekundu hao wa Msimbazi wamekuwa na uhakika wa kubeba ubingwa huo msimu huu baada ya kupata morali iliyochagizwa na Azam kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya Toto Africans na kuonekana kama imevuka ‘kigingi’ kimoja na aliyesalia kwa sasa ni Yanga.

Azam na Yanga ndizo ambazo zinaikosesha raha Simba ambayo ina kiu ya kutwaa ubingwa baada ya kushindwa kufanya hivyo kwa misimu mitatu mfululizo.

Licha ya Yanga kushinda katika mechi yake ya kiporo dhidi ya Kagera Sugar walipoibuka na ushindi wa mabao 3-1 Jumapili iliyopita, Simba bado wanaendelea kukaa kileleni mwa msimamo wakiwa na pointi 57.

Kabla ya michezo yao wikiendi iliyopita, Azam na Yanga walikuwa na viporo vitatu nyuma ya Simba ambapo Wekundu wa Msimbazi walikuwa wakiombea wapinzani wao hao wapoteze au kutoka sare ili wakae kileleni bila bughudha.

Katika maombi yao hayo walau yameanza ‘kutiki’ baada ya Azam kuwa tayari ameanza kupotea kwenye ramani ya ubingwa kwa sasa kwa kulazimishwa sare na Toto Africana wikiendi iliyopita.

Simba sasa wanaiombea Yanga nao kiporo chao kimoja kati ya viwili vilivyobakia kichache au vyote ili wawe na uhakika wa hesabu zao za ubingwa kutimia.

Simba wapo kileleni mwa msimamo wakiwa na pointi 57, baada ya kucheza michezo 24 wakifuatiwa na Yanga wenye pointi 53 katika michezo yao 22 waliyocheza sawa na Azam FC waliopo nafasi ya tatu na pointi zao 51.

Kama Azam watashinda viporo vyao viwili vilivyobakia, watafikisha pointi 57 na kulingana na Simba ambapo sasa itaangaliwa mwenye uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Kutokana na matokeo hayo ambayo Azam wameyapata sasa Simba wameelekeza akili zao zote kwa Yanga wakiomba kila aina ya dua ili wapate matokeo mabaya kwenye viporo vyao hivyo viwili.

Simba inataka kuitibulia Yanga katika viporo vyake viwili vilivyosalia ili asifikishe idadi ya pointi 59 endapo watoto hao wa Jangwani watashinda na kufuta ndoto zao za kubeba ubingwa.

Wekundu hao wana uhakika endapo Yanga itashinda mechi zote ataweza kufikisha jumla ya pointi 77 wakati Simba itamaliza ikiwa na pointi 75 huku Azam nao wakibaniwa leo na Ndanda watafikisha pointi 74.

Hivyo basi, Simba inahitaji kuzicheza mechi za viporo ambazo Yanga inataka kucheza ili iweze kujihakikishia kubeba ubingwa huo.

Yanga wamebakiwa na viporo viwili ambapo kama watapoteza kimoja kati ya hivyo ni wazi itakuwa faida kubwa kwa Simba, kwani watakuwa wakiendelea kutanua kileleni.

Wekundu hao wa Msimbazi wana misimu mitatu mfululizo bila kunusa harufu ya ubingwa na kushindwa kabisa kushiriki michuano ya kimataifa jambo ambalo linawakera sana na sasa wanataka msimu huu wafikie malengo yao.

Hesabu yao ni kuhakikisha wanatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na ule wa michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) ambayo bingwa wake anaiwakilisha nchi Kombe la Shirikisho Afrika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here