Home Habari SIMBA YAFANYA JEURI KAGAME

SIMBA YAFANYA JEURI KAGAME

7164
0
SHARE
NA MARTIN MAZUGWA        |

MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, leo watawakabili maafande wa JKU ya Zanzibar, mchezo wa nusu fainali ya michuano ya Kagame, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Simba wametinga hatua hiyo baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya AS Ports ya Djibout, mchezo wa robo fainali huku JKU wakiwatoa nishai Singida United, baada ya kuwafunga mabao 4-3 kwa changamoto ya mikwaju ya penalti.

Katika mchezo huo, Simba inaendelea kumtegemea straika wake mpya, Meddie Kagere ambaye amefunga mabao mawili katika michezo mitatu aliyocheza kwenye michuano hiyo.

Kagere anatarajiwa kushirikiana vizuri na straika mwenzake, Mohamed Rashid ambaye bao lake pekee dhidi ya AS Ports ndilo lililowavusha Simba hatua hiyo ya nusu fainali.

Akizungumzia mchezo huo, kaimu kocha mkuu wa timu hiyo, Masoud Djuma, alisema matarajio yake ni kuibuka na ushindi ili kutinga fainali na baadaye kutwaa ubingwa ambao unashikiliwa na Azam FC.

“Utakuwa mchezo mgumu kwani hata wapinzani wetu wamefika hatua hii baada ya kufanya kazi kubwa ila sisi tumejipanga kushinda, unajua tangu mwanzo tuliweka matumaini ya kutwaa ubingwa hivyo lazima tupambane,” alisema.

Taarifa nyingine zinazoenea chinichini kutoka ndani ya klabu hiyo kongwe zinadai kwamba, mashabiki wa klabu hiyo pamoja na wadau wengine wanauhitaji ubingwa wa  Kombe la Kagame kwa udi na uvumba ili watimize nia yao ya kufanya sherehe mbili kwa pamoja.

Sherehe hizo ni pamoja na ile ya ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara walioupata msimu uliopita pamoja na ubingwa wa Kombe la Kagame endapo watafanikiwa kutinga fainali na hatimaye kutwaa kombe.

“Kama tukitwaa ubingwa huu wa Kagame, tutafanya sherehe ya pamoja itakayojumuisha ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara tulioupata msimu huu,” alisema kigogo mmoja wa Simba.

Mchezo mwingine wa hatua hiyo ya nusu fainali ambao pia utachezwa leo, utawakutanisha mabingwa watetezi wa michuano hiyo Azam FC dhidi ya Gor Mahia ya Kenya.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa mkali kwa dakika zote, kwani mara ya mwisho timu hizo kukutana ilikuwa mwaka 2015 mchezo wa fainali na Azam FC kutwaa ubingwa na baada ya hapo michuano hiyo haikufanyika tena mpaka msimu huu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here