SHARE

NA CLARA ALPHONCE,

SIMBA hakuna kulala, kwani baada ya kupoteza mchezo wao dhidi ya Kagera Sugar, wakifungwa mabao 2-1, sasa wameshtukia mchezo mchafu uliofanyika na kusababisha kipigo hicho ambapo vigogo wote kwa umoja wao, wameamua kuungana na kwenda Mwanza kuweka kambi ya muda.

Kikosi hicho kimeongoza ligi kwa muda mrefu, lakini ghafla wakashtukia wanaenguliwa na watani zao wa jadi, Yanga, baada ya kupoteza dhidi ya Kagera Sugar na sasa wanaonekana hawataki utani tena katika michezo yao miwili iliyobakia ya Kanda ya Ziwa dhidi ya Mbao FC na Toto Africans.

Baada ya kupoteza mchezo huo, baadhi ya mashabiki na hata viongozi walianza kutoa lawama kwa baadhi ya  wachezaji kwa madai ya kucheza chini ya kiwango, kitu ambacho kimepelekea viongozi kutaka kuchukua maamuzi magumu ya kuwasimamisha ambao wanadaiwa kuhujumu.

Baada ya mjadala mrefu, vigogo hao kwa kauli moja wamekubaliana kusahau yaliyopita na sasa wameamua kujikita michezo yao hiyo miwili, wakianzia na Mbao FC Jumamosi ya wiki hii Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.

Mjumbe mmoja wa Kamati ya Utendaji ya Simba aliliambia DIMBA Jumatano kuwa baada ya vigogo wote wa Simba kukutana, walikubaliana kuacha kazi zao na kwenda Mwanza kwa ajili ya kuzuia hujuma nyingine, lengo likiwa kurudi na pointi sita zilizobakia Kanda ya Ziwa.

“Unajua timu ikifungwa katika mazingira ambayo hayaeleweki lakini kuwe na maswali mengi ya kujiuliza, lakini nipende tu kusema kwa umoja wetu tumeamua kupeleka nguvu kubwa jijini Mwanza kuhakikisha tunashinda michezo yetu miwili.

“Kitu tulichogundua ni kwamba, bado uwezekano wa kutwaa ubingwa upo, ila kinachotakiwa ni kuzidi kujenga umoja na mshikamano, kwani michezo mitano iliyobakia si michache,” alisema.

Pia mjumbe huyo alisema wamekubaliana viongozi kuwahoji wachezaji kama wana matatizo yoyote katika timu kabla ya mchezo wao ujao, ili kama kuna matatizo yaweze kufanyiwa kazi mapema.

Timu hiyo ipo Geita, ambako itakaa kwa siku kadhaa kabla ya kwenda Mwanza kwa ajili ya mchezo wao dhidi ya Mbao Jumatatu katika Uwanja wa CCM Kirumba.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here