Home Habari SIMBA YAFICHA MAJEMBE YAO SITA MAPYA

SIMBA YAFICHA MAJEMBE YAO SITA MAPYA

1990
0
SHARE

NA SAADA SALIM


ANAYEICHUKULIA Simba poa anaweza akaumbuka, kwani Wekundu hao wa Msimbazi wanaendelea na mambo yao kimya kimya na sasa wamefanikiwa kushusha vifaa sita vipya ambavyo wameviweka mafichoni kwa ajili ya kuvisajili.

Simba wanataka kuhakikisha wanaimarisha kikosi cha timu yao kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, na ili kulitimiza hilo tayari wamekwishawafanyia majaribio baadhi ya wachezaji kutoka ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kuwasajili kipindi hiki cha dirisha dogo.

Licha ya kwamba Wekundu hao wa Msimbazi wameanza mazoezi jana, lakini taarifa za uhakika zinadai kuwa, baadhi ya wachezaji wapya walikuwa mafichoni wakifanyiwa majaribio kwa siri katika Uwanja wa Chuo cha Ufundi Kurasini, jijini Dar es Salaam.

Taarifa hizo zinadai kuwa, waliokuwa wakisimamia mazoezi hayo ni kocha msaidizi Jackson Mayanja na meneja wao, Mussa Hassan ‘Mgosi’ na sasa anasubiriwa Kocha Mkuu, Joseph Omog, ili kupewa mrejesho.

Taarifa zaidi zinadai kuwa, wachezaji hao waliokuwa wakifanyiwa majaribio wapo sita, ambapo wenyewe Simba wanataka kuongeza mmoja au wawili na kuwajaribu wote, kisha wale watakaofanya vizuri, wanaweza wakaula.

DIMBA Jumatano lilifanya jitihada za kumtafuta Meneja wa Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’ , ili kuzungumzia suala hilo, lakini simu yake iliita bila kupokelewa, huku ile ya kocha msaidizi, Jackson Mayanja ikiwa bize muda wote.

Kikosi kamili cha Simba kilitarajiwa kuanza kufanya mazoezi jana katika Uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini, kwa ajili ya maandalizi ya mzunguko wa pili, wakitaka kuhakikisha msimu huu wanatwaa ubingwa.

Katika ripoti iliyoachwa na Omog ilihitaji kuongezewa wachezaji watatu, akiwamo kipa mmoja atakayempa ushindani Vincent Angban, ambaye hana mpinzani mwenye uwezo mkubwa pamoja na nafasi ya beki.

Pia kocha huyo amehitaji kuongezewa mshambuliaji mmoja mahiri kwa ajili ya kuongeza nguvu katika safu hiyo, ambapo wapo Laudit Mavugo, Ibrahim Ajib pamoja na Fredrick Blagnon.

DIMBA lilimtafuta Omog kwa simu, ambaye yuko nchini kwao Cameroon, ambaye alisema kwa sasa timu iko chini ya msaidizi wake, Mayanja na yeye ataanza rasmi kazi baada ya Ijumaa atakaporejea.

“Kwa sasa kikosi kipo chini ya Mayanja, nina uhakika baada ya kurejea Tanzania Ijumaa au Jumamosi nitaweka wazi kila kitu, ikiwamo mchezaji gani amesajiliwa,”  alisema Omog.

Alisema hata suala la mechi za kirafiki pamoja na sehemu watakayokwenda kuweka kambi timu hiyo itajulikana siku moja baada ya yeye kurejea.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here