Home Habari SIMBA YAHESABU POINTI TATU MTWARA

SIMBA YAHESABU POINTI TATU MTWARA

868
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU, MTWARA

SIMBA wanajua kuwa wapinzani wao wa jadi Yanga wamepanda kileleni baada ya kuwafunga JKT Ruvu mabao 3-0 jana na sasa Wekundu hao wa Msimbazi wameapa kurudi kwenye nafasi yao hiyo.

Simba ambao wana pointi 35, wameongoza ligi kwa muda mrefu lakini wamejikuta wakiondolewa kileleni na Yanga baada ya Wanajangwani hao kufikisha pointi 36 kutokana na ushindi huo wa jana.

Wekundu hao wa Msimbazi wanashukuka katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona Mkoani hapa kucheza na Ndanda FC ambapo kama wakishinda watafikisha pointi 38 na kurudi kileleni.

Simba wanashuka katika mchezo huo wakizisaka pointi zote tatu ili kuhakikisha ndoto zao za kutwaa ubingwa msimu huu zinatimia.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza timu hizi zilipokutana Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Simba waliibuka na ushindi wa mabao 3-1 huku wakionyesha kandanda la kuvutia.

Simba wanayo historia nzuri ya ushindi wanapokutana na timu hii ambapo mashabiki wao wanaamini kuwa dakika 90 zitakapomalizika leo wataendeleza furaha yao.

Akizungumzia mchezo huo Kocha Mkuu wa Wekundu hao wa Msimbazi Joseph Omog, alisema kikosi chake kimekalimika kila idara na kwamba wanachoangalia ni kuondoka na pointi zote tatu na wala siyo kitu kingine.

“Kwanza niseme hautakuwa mchezo rahisi kwani hata wapinzani wetu wanazihitaji hizo pointi tatu lakini yote kwa yote sisi tumejipanga vizuri na tunataka kuwafurahisha mashabiki wetu ambao wana hamu kuiona timu yao ikishinda.

“Tuliuanza mzunguko wa kwanza vizuri tukaja kufungwa mechi mbili za mwisho lakini sasa tunataka kuhakikisha hatupotezi mchezo wowote mpaka ligi itakapomalizika,” alisema.

Kwa upande wake meneja wa kikosi hicho Mussa Hassan ‘Mgosi’ alisema msimu huu ni wao na lazima watwae ubingwa ambo wameusubiria kwa misimu minne mfululizo ambapo leo wataondoka na pointi tatu.

“Kama tulivyosema kabla hata ligi haijaanza kwamba msimu huu tumedhamiria kutwaa ubingwa, bado msimamo wetu upo palepale na mchezo wetu dhidi ya Ndanda (leo) tutahakikisha tunashinda,” alisema.

Katika mchezo wa leo Simba itawategemea zaidi wakali wake kama Shiza Kichuya, Ibrahim Ajib, Laudit Mavugo, Jonas Mkude, Mzamiru Yassin na wengine.

Mbali na mchezo huo, michezo mingine ambayo itachezwa leo Azam FC watacheza na African Lyon Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, Tanzania Prisons watawakaribisha Majimaji Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya na Mbao FC watacheza na Stand United Uwanja wa CCM Kirumba.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here