SHARE

NA SAADA SALIM,

BAADA ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutangaza ratiba ya nusu fainali ya Kombe la FA, kwamba Simba itakutana na Azam FC, Kocha wa Wekundu hao wa Msimbazi, Joseph Omog, ameonyesha jeuri kubwa baada ya kusema hana presha kabisa na wapinzani wao hao.

Tayari Wekundu hao wa Msimbazi wameweka kambi Chuo cha Biblia eneo la Bigwa, mkoani Morogoro, chini ya kocha Mcameroon huyo, Omog, kujiandaa na mchezo huo wa nusu fainali unaotarajiwa kupigwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Omog ameliambia DIMBA Jumatano kwamba, timu yake ipo vizuri na hana presha kabisa na wapinzani wao hao, akiamini kuwa vijana wake watapambana na kupata ushindi utakaowawezesha kutinga hatua ya fainali.

“Niseme tu kwamba, Azam ni timu nzuri, lakini haimaanishi kuwa tunawaogopa wala haimaanishi watatufunga, maandalizi yetu yako vizuri sana na nina imani kuwa tutawafunga na tutaingia fainali,” alisema.

Alisema wachezaji wake wote wapo fiti, isipokuwa Method Mwanjali, ambaye anaendelea kuuguza majeraha yake, hiyo ikimaanisha kuwa safu ya ulinzi itawategemea zaidi Abdi Banda pamoja na Juuko Murushid.

Hii itakuwa mara ya nne Simba kukutana na Azam FC msimu huu, kwani mara ya kwanza walikutana mchezo wa Ligi Kuu mzunguko wa kwanza Simba wakashinda bao 1-0, likifungwa na Shiza Kichuya, na mchezo wa pili wakakutana katika fainali michuano ya Kombe la Mapinduzi na Azam wakashinda bao 1-0, lililofungwa na Himid Mao kwa shuti kali.

Mara ya tatu timu hizo zilikutana mchezo wa Ligi Kuu mzunguko wa pili ambapo Azam FC kwa mara nyingine wakawafunga Simba bao 1-0, lililofungwa na nahodha John Bocco, akimzidi ujanja beki Method Mwanjali na kuukwamisha mpira wavuni.

Rekodi hizo zinaonyesha kwamba, msimu huu Azam wamewaonea Simba na kama Wekundu hao wa Msimbazi watafanikiwa kuibuka na ushindi, watakuwa wamelingana, kila mmoja akimfunga mwenzake mara mbili.

Mshindi katika mchezo huo atakutana na mshindi kati ya Yanga na Mbao FC, mchezo utakaochezwa Jumapili ya wiki hii Uwanja wa CCM Kirumba na kama Azam atashinda na Yanga wakashinda, inamaanisha kuwa historia ya msimu uliopita itajirudia, ambapo timu hizo zilikutana fainali na Yanga kuibuka kidedea.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here