Home Habari SIMBA YAINASA ROHO YA AS VITA

SIMBA YAINASA ROHO YA AS VITA

0
SHARE

NA CLARA ALPHONCE

KAMA ulidhani bilionea wa Simba, Mohamed Dewji (Mo), alivyosema anataka msimu ujao aisuke kisasa timu hiyo anatania bila shaka hujui kinachoendelea kwani ndiyo kwanza mambo yameanza kusukwa.

Taarifa za ndani kutoka Simba zinadai kwamba, bilionea huyo amevutiwa na uwezo mkubwa alionao kocha mkuu wa AS Vita ya DR Congo, Florent Ibenge na mipango ya kumsogeza karibu imeshaanza kusukwa.

Kocha huyo ambaye pia anaifundisha timu ya Taifa ya Congo akisaidiwa na Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, ni moja ya makocha wenye mbinu kali uwanjani hivyo Simba wakimnasa watakuwa wamelamba dume.

Taarifa hizo kutoka Simba zinadai kuwa huenda msimu ujao wakaachana na Patrick Aussems, hivyo chaguo la kwanza la Mo Dewji ni kocha huyo wa AS Vita, baada ya kufurahishwa na kazi nzuri anayoifanya.

“Hii mipango inasukwa chini kwa chini kwani jamaa (Mo Dewji) amedhamiria kuifanya Simba iwe inatisha zaidi ya hapa ilipo na kwa kuanzia anafikiria kumshusha nchini kocha wa AS Vita kutokana na kuvutiwa na kazi yake,” alisema kigogo mmoja ndani ya Simba.

Alisema mbali na kocha huyo, pia wapo wachezaji wawili kutoka kikosi hicho cha AS Vita, ambao wameshanasa kwenye rada za Mo na huenda nao wakatua kwa ajili ya msimu ujao.

“Mbali na huyo kocha, pia wapo wachezaji wawili ambao kwa sasa ni vigumu kukutajia majina yao, lakini kwa namna mambo yanavyokwenda bila shaka tutakuwa nao msimu unaokuja,” alisema.

Licha ya kwamba alikataa kutaja majina ya wachezaji hao lakini DIMBA linajua kwamba Wekundu hao wa Msimbazi, wamerudisha upya mbio zao za kumfukuzia, Jean Marc Makusu Mondele, ambaye ni kinara wao wa kupachika na ndiye pia aliwasumbua sana Simba kwenye ushindi wa mabao 5-0.

Kama Simba watafanikisha mpango huo, hilo litakuwa pigo kubwa kwa AS Vita kwani kocha huyo ndiye tegemeo lao kubwa lakini pia wachezaji hao wawili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here