Home Michezo kitaifa SIMBA YAIPASUA TP MAZEMBE

SIMBA YAIPASUA TP MAZEMBE

1932
0
SHARE

SAADA SALIM NA EZEKIEL TENDWA

BAADA ya kujikuta wakiangukia mikononi mwa Simba hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika, uongozi na benchi la ufundi la TP Mazembe ya DR Congo, wanahaha kutaka kujua kwanini Wekundu hao wa Msimbazi wanakuwa na kiburi cha kushinda uwanja wao wa nyumbani kila mechi.

Mazembe wanajua kuwa wenzao AS Vita, walikiona cha moto wakifungwa mabao 2-1 Taifa na kutupwa nje ya michuano hiyo na sasa wanatafuta mbinu za kuwazidi ujanja Wanamsimbazi hao.

Mbali na Vita, pia timu kama Al Ahly ya Misri pamoja na JS Saoura ya Algeria, nazo zilijikuta zikidondosha pointi Uwanja wa Taifa na kuzua hofu kwa timu nyingine hasa Mazembe.

Taarifa kutoka Congo zinadai kuwa ushindi huo wa Simba uwanja wao wa nyumbani ikizifunga timu vigogo, umelifanya benchi la ufundi la Mazembe, kugawana majukumu kila mmoja akitakiwa kuingia msituni kuwachunguza Wekundu hao wa Msimbazi.

Mtanzania mmoja anayeishi Congo, ameliambia DIMBA kuwa Mazembe wameingiwa na hofu wakijua kwamba yanaweza yakawakuta kama ilivyotokea kwa wenzao AS Vita ndiyo maana wameanza kujipanga mapema.

“Huko Tanzania watu wanaweza wakaichukulia kirahisi Simba, lakini huku hali ni mbaya sana, mashabiki wa TP Mazembe wanaiona timu yao kwamba imepungua makali na wanaamini huenda wakafungwa.

“Taarifa zilizopo ni kwamba, benchi lao la ufundi limegawana majukumu kila mmoja akitakiwa kuipeleleza Simba na kuijua ndani na nje, kujua wachezaji wao wakali na wapi ambapo ni dhaifu, nadhani Simba wakijipanga vizuri wataishangaza Afrika,” alisema.

Kwa upande wa Simba, Ofisa Mtendaji wao Mkuu, Crescentius Magori, alisema maandalizi yanaendelea vizuri, viongozi  wanatarajia kukutana mara baada ya kumalizika kwa mechi ya Taifa Stars dhidi ya Uganda leo huku akidai watatinga nusu fainali.

“Tumegundua tatizo lilikuwa kufungwa mabao mengi tunapokwenda ugenini sasa hilo kocha analishughulikia maana lipo kwenye uwezo wake kuwapanga vijana vizuri ili tufanye kama nyumbani.

“Niwahakikishie Wanasimba wote kwamba sisi viongozi hatulali na badala yake tunafanya kila linalowezekana kushinda, hata sasa tunasubiri mchezo wa Stars dhidi ya Uganda umalizike tukutane tena,” alisema.

Alisema uongozi tayari umeandika barua Bodi ya Ligi kuomba baadhi ya michezo yao kusogezwa mbele ukiwemo wa Machi 3, 9 na 12 mwaka huu na kutaka kutumia muda huo kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wao dhidi ya TP Mazembe utakaopigwa Machi 6.

SHARE
Previous articleNI ZAMU YETU
Next articleKIGOGO YANGA AACHIA NGAZI

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here