SHARE

NA MAREGES NYAMAKA-MBEYA

BAADA ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City, mchezo uliopigwa Jumamosi, Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Simba leo itaingia kivingine kuivaa Prisons, katika uwanja huohuo, mjini hapa.

Jana kikosi cha Simba chini ya kocha wake mkuu, Patrick Aussems kilifanya mazoezi mepesi kwa muda wa saa mbili na kisha kwenda katika mapumziko kwa ajili ya kujiandaa na mechi hiyo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Tofauti na ilivyokuwa katika mechi ya Mbeya City, Kocha Aussems aliliambia Dimba kwamba, anahitaji kufanya mabadiliko kidogo na pia kuongeza kasi ya mchezo ili kuweza kutafuta ushindi dhidi ya timu hiyo ambayo ameitaja kuwa ni ngumu.

Katika mchezo huo, Simba itawakosa mabeki wake wa kuaminika, Paul Bukaba na Jjuuko Murshid, walioumia katika mchezo dhidi ya Mbeya City.
Akizungumzia tofauti ya Prisons, Aussems alisema anaiheshimu timu hiyo na anaifahamu uwezo wake, hivyo amekitengeneza kikosi chake ili kicheze kulingana na mchezo wa timu hiyo.

“Tulicheza nao mechi ya fungua dimba, michuano ya Ligi Kuu, tukapata ushindi wa bao 1-0, ilikuwa mechi ngumu, pia nimeangalia mechi zao nyingi hata hii dhidi ya Yanga ni timu ngumu inahitaji mikakati haswa,” alisema.

Katika hatua nyingine, kocha huyo alilalamikia tabia inayoanza kuibuka kwa waamuzi ambao wamekuwa wakiogopa kuchezesha mechi zao kwa kufuata sheria, wakihofia kufungiwa kama ilivyokuwa kwa mwenzao aliyechezesha mechi yao dhidi ya KMC.

“Wanachotakiwa ni kutafsiri sheria 17 kwa umakini uwanjani na si kuogopa mechi za Simba, watakuwa hawatutendei haki,” alisema.

Wakati huohuo, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Haji Manara, amewataka Wanasimba kupuuza kauli zinazotolewa kwamba timu yao inashinda mechi zake kwa kusaidiwa na siyo kwa uwezo wa wachezaji.

Manara alizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana na kusema kwamba, Simba ina kikosi kipana na imejipanga kushinda mechi zake za ligi, hivyo wanachofanya wachezaji ndicho walichoandaliwa kukifanya na benchi la ufundi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here