SHARE

>>Mo aagiza CAF ukamilike fasta

NA WINFRIDA MTOI

SIMBA imecharuka, imeamua kufanya kweli katika kutekeleza agizo la Shirikisho la Soka Afrika(CAF), kwa vitendo.

Hiyo ni baada ya kuanza kushusha vifaa vipya na kuwaongezea mikataba mipya wachezaji wake wanaoona wanastahili kuendelea kuwepo katika kikosi hicho.

Kabla ya Kocha wa Simba Patrick Aussems hajakwenda mapumziko, alisema anahitaji usajili wa wachezaji watano wa kimataifa na moja ya sifa wawe wametoka katika timu bora zilizofanya vizuri katika michuano ya Afrika.

Juzi Wekundu wa Msimbazi hao, walianza kwa kuweka wazi kuwa imemuongezea mkataba wa miaka miwili mkali wao wa mabao John Bocco na jana ilikuwa ni zamu ya Aishi Manula aliyeongeza mkataba wa miaka mitatu.

Wachezaji hao wote ambao wako katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, walithibishwa na uongozi wa kikosi hicho pamoja na picha zilizowanyesha wakiwa wanasaini mbele ya mwekezaji wa klabu hiyo, Mohammed Dewji ‘Mo’.

Usajili huo unaofululiza ni klabu hiyo kutaka kukamilisha mapema uboreshaji wa kikosi hicho baada ya CAF kutoa tarehe ya mwisho ya kupeleka majina ya vikosi vitakavyoshiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.

Kwa mujibu wa CAF, kila timu inayotarajia kushiriki michuano hiyo mwaka huu, inatakiwa kukamilisha usajili wake mapema mwisho wa mwezi huu.

Kutokana na hilo, inadaiwa kuwa mwekezaji wa Klabu hiyo, Mohammed Dewji ‘Mo’ ameagiza usajili wa CAF ufanyike haraka iwezekanavyo ili kutengeneza kikosi imara kitakachokuwa na ushindani, pia kubadilisha ripoti ya kocha iliyotaka kuacha wachezaji watano wa kimataifa na sasa watandoka watatu tu.

Watakaopewa mkono wa kwaheri hivi sasa ni pamoja na Mghana Asante Kwasi, Nicolaus Gyn na Zana Collbary.

Katika hilo kutekeleza suala hilo, inasemekana tayari uongozi wa Simba umemalizana na robo tatu ya wachezaji wao waliokuwa wamemaliza mikataba kwa kuwaongezea mipya.

Wachezaji ambao tayari Simba imeshawatia vitanzi ni, John Bocco, Aishi Manula, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Shomali Kapombe na wengine.

Pia DIMBA limepata taarifa za ndani kuwa miongoni mwa wachezaji wazawa, Ibrahim Ajib yumo ndani ameshasaini, kilichobaki ni kukabidhiwa kitita chake cha fedha.

Tofauti na maboresho ya kikosi, Kocha Mkuu Patrick Aussems, atakatiza likizo yake ili kurejea mapema kufanya maandalizi na kukamilisha usajili huo.

Akizungumzia suala hilo, Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Klabu ya Simba, Crescentius Magori, alikiri kuwepo katika mchakato wa usajili na kuwaongezea mikataba mipya wachezaji wao.

Magori alieleza kuwa muda wowote watakapomaliza na mchezaji wataweka wazi kama walivyofanya kwa John Bocco na Aishi Manula.

“Kila kitu kinachoendelea juu ya usajili na maboresho ya kikosi chetu kitawekwa wazi, kwa sababu tayari tumeshapitia ripoti ya mwalimu na kujua mahitaji yake,” alisema Magori.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here