Home Habari SIMBA YAMTHIBITISHA RASMI NIYONZIMA

SIMBA YAMTHIBITISHA RASMI NIYONZIMA

0
SHARE

NA SAADA SALIM

WAKATI Yanga wakihangaika kuziba pengo la kiungo Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, anayetajwa kutimkia Simba, Wekundu hao jana wamethibitisha rasmi hadharani kuwa imemalizana naye na wakati wowote kuanzia sasa mashabiki watamuona akiwa na uzi wenye rangi nyekundu na nyeupe.
Tangu kuwepo na habari za kusajiliwa kwa Niyonzima, Simba ilikuwa haijaweka rasmi taarifa sahihi kama ni kweli amesajiliwa ama la na hivyo kuwaacha mashabiki wengi katika maswali, wengine wakidhani hilo ni changa la macho.
Hata hivyo jana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba, Haji Manara, alisema wameshakamilisha usajili wa Niyonzima baada ya mkataba wake na Yanga kumalizika na atatua nchini mwishoni mwa wiki kujiunga na timu tayari kwa Tamasha la Simba Day, linalotarajiwa kufanyika Agosti 8, mwaka huu.
Niyonzima amemaliza mkataba na Yanga ambapo klabu yake hiyo ya zamani ilithibitisha kutoendelea naye mara baada ya mchezaji huyo kugomea uongozi wa timu hiyo kuongeza mkataba mpya, huku ikidaiwa kasaini Simba mkataba wa miaka miwili.
Takribani miezi miwili iliyopita zilisambaa taarifa kuhusu kiungo huyo fundi kusajiliwa na Simba, lakini si yeye wala klabu hiyo ya Msimbazi waliokuwa tayari kuliweka wazi suala hilo, wakisubiri mkataba wake na Yanga umalizike mwishoni mwa Julai, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Manara alithibitisha juu ya ujio wa kiungo huyo, kwamba ni mchezaji rasmi wa Simba na muda wowote ataungana na timu hiyo na kutambulishwa rasmi katika tamasha lao la Simba Day.
“Niyonzima ni mchezaji wetu halali, kuna mawili ataungana na wenzake Kigali, Rwanda wakati timu itakapofika hapo kuunganisha ndege wakitokea Afrika Kusini au kutangulia kufika kabla ya kikosi cha Simba hakijawasili nchini,” alisema.
Manara alisema Niyonzima alikuwa na ruhusa maalumu baada ya kuripoti kuwa na matatizo ya kifamilia na hivyo kuendelea kufanya mazoezi katika timu yake ya zamani ya APR ya Rwanda.
Alisema Mnyarwanda huyo, kipa mpya aliyejiunga na timu jana, Aishi Manula pamoja na wachezaji wengine kadhaa wanaratajiwa kutambulishwa rasmi katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda, siku ya Simba Day.

Yazindua wiki ya Simba
Mbali na ishu ya Niyonzima, Manara alisema klabu hiyo imezindua rasmi wiki yake ijulikanayo kama (Simba Week) jana, kuelekea kilele cha maadhimisho ya sherehe kubwa ya timu hiyo inayofanyika kila mwaka, ikijulikana kwa Simba Day, inayofikia tamati Agosti 8.
“Sherehe hizo zitakuwa kubwa, ikiwa ni mara ya pili baada ya mwaka jana kuizindua rasmi wiki ya Simba, ambapo kutakuwa na matukio mbalimbali kuanzia leo,” alisema.
Manara alisema leo viongozi wa klabu hiyo kwa kushirikiana na baadhi ya wanachama watazindua rasmi tamasha lao mtaa kwa mtaa, ambapo watatembelea baadhi ya mitaa, pia Agosti 3 watakwenda kutembelea wachezaji wa zamani ambapo mwaka jana walikwenda kumtembelea Abdallah Kibadeni nyumbani kwake.
“Hii ni desturi yetu ya wiki ya Simba, siku ya Ijumaa viongozi wa klabu watakuwa na ziara ya kwenda kutembelea watoto yatima na kutoa sadaka, ambapo Jumamosi kikosi kizima cha Simba kilichoko Afrika Kusini, kitarejea nchini,” alisema.

Kontena 12 jezi ya Niyonzima zatua
Wakati maandalizi ya kuelekea Simba Day yakizidi kupamba moto, kuna taarifa kuwa Simba wanatarajia kufanya biashara katika tamasha hilo kupitia jezi za Niyonzima pamoja na Manula, ambao wamekuwa ngumzo kutokana na mikataba yao.
Tayari kontena za jezi hizo zimetua ambapo katika tamasha hilo klabu hiyo itahakikisha inatumia vyema kuuza jezi za wachezaji wao, huku wakihakikisha kupambana na wanaouza jezi feki.

Jjuuko Murshid na Orlando Pirates:
Kuna taarifa kwamba beki wa Simba, Jjuuko Murshid, anatakiwa na klabu ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini, lakini kwa mujibu wa Manara, bado pande hizo mbili zinaendelea na mazungumzo juu ya mkataba.
“Kwa sasa bado tuko naye katika mazungumzo ya kumuongeza mkataba, kama hiyo klabu itakuja kwetu kuhitaji huduma ya mchezaji wetu hatutakuwa na pingamizi,” alisema Manara.
Alisema kuwa, Simba haitakuwa tayari kumzuia mchezaji atakayepata ofa nzuri ya kucheza soka nje ya Tanzania, na wao watakuwa tayari kumuachia beki huyo kama viongozi wa klabu hiyo ya Afrika Kusini watafanya mawasiliano na klabu hiyo ya Wekundu wa Msimbazi.

Ujio wa Rayon Sport
Msemaji huyo alisema timu ya Rayon Sports ya Rwanda watakayocheza nayo mechi siku ya Simba Day, itawasili Agosti 7, mwaka huu na ndege ya Shirika la Ndege la Rwanda, kabla ya siku ya pili kucheza mechi na Simba Agosti 8, katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Alisema katika tamasha hilo pia kutakuwa na baadhi ya mechi za ufunguzi ambapo timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20, timu ya viongozi na wachezaji wa zamani pamoja na kikosi cha timu ya wanawake ya (Simba Queens) zitacheza, huku wakitarajia leo kutangaza wapinzani wa timu hizo tatu.
“Kuhusu viingilio pia tutavitangaza kesho (leo) tutakapozindua uuzaji wa tiketi za awali ambazo mtu atakayezinunua mapema atapunguziwa bei, ila kwa wale watakaonunua siku ya mechi viingilio itakuwa bei ya juu zaidi,” alisema Manara.

Omog anena
Kutoka kambini Afrika Kusini, Kocha wa klabu hiyo, Joseph Omog, alisema kikosi chake kipo vizuri na kila mmoja aliyekuwapo ndani ya kambi hiyo amewapa majukumu yao.
“Nimeona viwango vya wachezaji wote niliokuwa nao hapa nchini, ukiangalia safu yangu ya ushambuliaji kila mmoja nimewapa majukumu yake, kikubwa ni kuhakikisha tunapata idadi kubwa ya mabao, hali iliyopelekea nikahitaji mastraika wengi,” alisema.
Omog alisema hawezi kuzungumza kiwango cha mchezaji mmoja mmoja, kwani tayari kila mchezaji anatambua jukumu lake, hivyo kila mchezaji atapata muda wa kucheza mechi za kirafiki ili kuangalia kombinesheni na mawasiliano kati yao.
“Tunacheza mechi mbili hapa Afrika Kusini, tutarejea nyumbani kucheza mechi nyingine za kirafiki, ikiwamo ya Simba Day na nyingine, hizi zitanisaidia kupata kikosi cha kwanza kulingana na kombinesheni za wachezaji wangu,” alisema Mcameroon huyo.
Mbali na mechi hizo, pia Simba itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro, ikiwa ni mechi ya kirafiki, lakini itakuwa muhimu kwa ajili ya kuchangia damu.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here