SHARE

NA MAREGES NYAMAKA

SHIRIKISHO la Soka Barani Afrika(CAF)limeanika ratiba ya kuanza kwa michuano ya ngazi ya vilabu, Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

Ratiba inaoonyesha mechi za michuano hiyo zitaanza kupigwa kati ya Agosti 9/10/11 tofauti na ilivyokuwa huko nyuma ambapo timu zilitoka ligi za ndani tayari zikiwa zimecheza zaidi ya mechi 10.

Kuachiwa ratiba hiyo kumewafungua macho wawakilishi wa Tanzania katika michuano hiyo Simba,Yanga Azam na KMC kuwajua wapinzani ili kuwasoma fasta kabla ya kukabiliana nao.

Msimu huu asilimia kubwa ya timu zinavaana zote zikiwa hazijaanza kucheza ligi ya ndani ambayo mbali na kila timu kusaka ubingwa imekuwa ikitumika kama sehemu ya maandalizi ya michuano hiyo yenye kutoka mkwanja wa nguvu.

Simba wapo kambini Afrika Kusini ni mwendo wa mazoezi ya gym pamoja na uwanjani, bahati nzuri zaidi wana mechi nne za kirafiki miongoni mwa timu hizo kuna Orland Pirates.

Kocha wao ni yule yule, Patrick Aussems ambaye wachezaji waliompa matokeo bora msimu uliopita kwenye michuano hiyo asilimia 85 bado wapo kikosini hapo. Sioni presha ya kuwavaa US do Songo.

Yanga ni wiki tatu sasa wapo Morogoro wanajifua, miili ya wachezaji iko tayari kwa kazi na kasi inayotakiwa. Wanahitaji mechi mbili hadi tatu za nguvu kimataifa ili kujiweka sawa.

Idadi kubwa ya wachezaji wana uzoefu na mchuano.

Ni uwajibikaji tu sammbamba na nidhamu ya mchezo na mbinu za kocha, Mwinyi Zahera kuwakabili Township Rollers iliyowatesa 2018.
Kila mchezaji aliyesajiliwa Yanga siku anasaini mkataba alishatambua timu inahitaji nini kutoka kwake, ikiwamo michuano hiyo yenye thamani kubwa zaidi.

Kujiandaa kunaanzia kichwani halafu inafuata miguu na kichwa ambavyo vinajaziwa mbinu na kocha.Azam chini ya kocha mpya, Etienne Ndairagije, michuano ya Kombe la Kagame imewajenga wachezaji wake na yeye mwenyewe. Ilikuwa sehemu ya maandalizi. Kucheza michezo zaidi ya sita yenye ushindani mkubwa, wachezaji wameingiza kitu mwilini na akilini.

Kupata kwa matokeo bora mbele ya timu kama TP Mazembe pamoja na ndugu zao, Maniema Union wachezaji wameingiza kitu, lakini pia ilikuwa sehemu sahihi ya kocha kuaangalia zaidi upungufu kuliko ubora.

Katika wiki kadhaa zilizobaki kocha ana nafasi ya kuyafanyia kazi mapungufu kabla ya kuwafuata Ethiopia Bunna iliyomaliza nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi msimu uliopita.

Ethiopia Bunna bado wanaonekana wasiwe mlima mrefu kwa Azam. Mara mwisho kushiriki Kombe la Shirikisho ilikuwa 2004 ambapo waliishia hatua ya awali, huku mafanikio yao makubwa yakiwa ni kufika raundi ya pili 2000 na 2001.

Upande wa KMC ambao ni wageni kabisa kwenye hii michuano, huenda pia michuano ya Kagame ikawa hatua ya awali namna michuano ya kimataifa inavyochezwa. Nahodha, Yusuf Ndikuma anaamini katika hilo.

Kikosi hicho chini ya kocha Mganda, Jackson Mayanja tiketi yake ya kuendelea kuonekana raundi inayofuata ipo mikononi mwa AS Kigali ya Rwanda. Matumizi mazuri ya Uwanja wa nyumbani, Taifa au Uhuru ndo kitu muhimu kuliko chochote.Narudia tena maandalizi yaanzia kichwani baadaye miguuni.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here