Home Habari SIMBA, YANGA KIMENUKA ZENJI

SIMBA, YANGA KIMENUKA ZENJI

455
0
SHARE

NA EZEKIEL TENDWA

KIMENUKA! Wababe wa soka nchini, Simba na Yanga, wanakutana Jumatano ya Agosti 23, katika mechi ya Ngao ya Jamii kuashiria kufunguliwa kwa pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na sasa kama kawaida yao wameanza kuviziana, huku kila upande ukipanga kuipeleka timu katika visiwa vya Zanzibar.

Katika mechi tatu za Ligi Kuu Bara zilizopita kati ya nne, dhidi ya watani zao Yanga, Simba ilikuwa ikitokea mkoani Morogoro na hakuna iliyoibuka na ushindi, jambo lililowashtua viongozi wake na fasta wakaamua kufanya mambo ili kurekebisha upepo.

Mabosi wa Simba wakabaini kuwa ni ngumu kwao kupata matokeo kama itaendelea kuweka kambi yao mjini Morogoro na hivyo kuamua kubadili gia angani na kuhamishia kambi kisiwani Unguja, ambako wana bahati wanapoweka kambi kuwakabili Yanga.

Watani zao, Yanga, waliokuwa na mechi ya majaribio jana dhidi ya Ruvu Shooting na kuambulia kichapo cha bao 1-0 kwenye Uwanja wa Chamazi, wamepanga kuondoka leo Jumapili kwenda kisiwani Unguja, kucheza mechi moja ya kirafiki na baadaye kutimkia Pemba, kuwakimbia wapinzani wao hao.

Kwa upande wao Simba, wamebaini kuwa kambi ya Morogoro ilikuwa ikiwabeba Yanga, ndiyo maana ukiacha mechi ya mwisho ya ligi msimu uliopita waliposhinda 2-1, mechi zao tatu zilizopita, mbili walipoteza kwa 2-0, kabla ya kuambulia sare ya 1-1 katika mechi ya mzunguko wa kwanza msimu uliopita na safari hii wameapa lazima kieleweke tena, wakienda Unguja.

Hata hivyo, Yanga ndio waliokuwa wa kwanza kusema wanakwenda Pemba kuweka kambi, wakati Simba wakidaiwa wangekwenda Morogoro, lakini ghafla nao wakabadili nia na kuamua kwenda kujificha Unguja, safari ambayo inaanza kesho Jumatatu.

Simba wanacheza leo mchezo wa kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar, Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam na baada ya hapo watakwenda kujiandaa kwa safari hiyo kesho.

Taarifa kutoka Zanzibar zinadai kuwa, wanachama na mashabiki wa pande zote wamejiandaa kuzipokea timu zao hizo, huku wakiahidi kuzilinda ili kuepuka hujuma za kila aina, kuelekea mchezo huo.

Akizungumza jana kutoka Unguja, shabiki mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Omary Hussein, alisema wanaisubiri kwa hamu timu yao ya Simba na kwamba wamejipanga kuhakikisha hakuna mamluki atakayeweza kujipenyeza na kusoma mbinu zao.

“Nasikia wenzetu (Yanga) wanakwenda Pemba, ila sisi kama mashabiki wa Simba tunasema tumejiandaa kuipokea timu yetu na kuipa kila aina ya ushirikiano na hakuna mamluki yeyote atakayeweza kujipenyeza,” alisema.

Kwa upande wa Pemba, Issa Omary Yusuph alisema wanaikaribisha timu yao ya Yanga kwa mikono miwili na kama kuna mtu yeyote aliyejiandaa kuihujumu timu yao itakula kwake, kwani ulinzi upo wa kutosha.

“Yanga huku ni nyumbani kwao na wenyewe wanajua kwamba wanapokuja huku ulinzi unakuwa imara, niwahakikishie mashabiki wenzetu wa Dar es Salaam kwamba hakuna kitakachoharibika huku,” alisema.

Msemaji wa Simba, Hajji Manara, alisema kikosi chao kinaondoka kesho ambapo kitarudi siku moja kabla ya mchezo, huku Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa, akisema timu yao itarejea Agosti 21, yaani siku mbili kabla ya mchezo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here