SHARE

NA ABDUL MKEYENGE

WIKI iliyopita mitandaoni na kwenye vyombo vya habari kulikuwa na kelele nyingi za mashabiki wa Simba wakifurahia timu yao kwenda Mbeya kwa ajili ya michezo miwili ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons. Simba wameenda jijini humo kwa usafiri wa anga na mashabiki wake wamefurahi kwelikweli.

Hata Yanga nao huwa wanasafiri kwa usafiri huo kwa baadhi ya mikoa kwa ajili ya michezo ya Ligi Kuu Bara. Na Yanga nao wakitumia usafiri huo mashabiki wake nao wanafurahi kwelikweli.

Inashangaza hapa! Hivi bado tunaishi dunia ya Simba, Yanga zikitumia usafiri wa anga mashabiki wake wanaona kitu kikubwa kinachowafanya wakifurahie? Tunaishi dunia ya ajabu sana.

Muda mrefu nimechunguza suala hili na nimegundua kuna shida kwenye soka letu. Kuna baadhi ya shida zinatokana nasi waandishi kuandika taarifa zinazopendwa na walaji wetu ambao ni wasomaji.

Ni ngumu waandishi kuliepuka hili, lakini nasi (waandishi) tunapelekwa na upepo wa wasomaji ulivyo. Binafsi sikutaraji kama taarifa za Simba, Yanga kutumia usafiri wa anga kwa safari zao kingekuwa kitu kikubwa kinachozungumzwa kila pembe. Nilifikiri tofauti juu ya hili.

Lakini kwa kasi ya mazungumzo na mikogo iliyoko mitandaoni hivi sasa baada ya Simba kwenda Mbeya kutumia usafiri huo, imekuwa stori kubwa inayozungumzwa kila sehemu. Kichekesho zaidi mashabiki wa Yanga wamenywea. Wanajisikia vibaya wenzao kupanda ndege kwenda Mbeya.

Mpira wa Tanzania ni wa ajabu sana. Soka letu ni zaidi ya tunavyolifikiri kuwa siku moja linaweza kufika kirahisi kwenye nchi ya ahadi ambayo kila Mtanzania anaiota nchi hiyo.

Lakini kumbe tuna mambo mengi ya kujifunza nje ya soka lenyewe kabla ya kuifikia nchi hiyo. Inashangaza stori za usafiri wa anga kupewa kipaumbele kuliko stori nyingine ambazo watu walipaswa kuzijua kuwa Simba, Yanga zimefanya kitu gani kikubwa zaidi ya kupanda ndege.

Simba, Yanga ni timu kubwa. Kwao kutumia usafiri wa anga kwenda kokote pale ni jambo la kawaida na la kupuuzwa. Ingekuwa stori kubwa kama tungeona timu hizo zinamiliki ndege zao kwa matumizi ya safari zao, lakini kutumia ndege kwa muda kisha timu inarudi kwenye maisha yake ya kawaida, si kitu cha kushangiliwa na kuwafanya mashabiki watoke mishipa ya shingo kwa kubishana.

Simba, Yanga zilipaswa kuwa na taarifa nyingi za maana ambazo zingekuwa mabalozi wazuri kwa timu nyingine za ndani na wao wajifunze kutokea kwa timu hizo kubwa.
Lakini haiko hivi ndiyo kwanza kiongozi akiwa na uhakika na timu yake kusafiri kwa njia ya anga, anatamba akiwa anazungumza na vyombo vya habari vinavyokuwa vimemzunguka. Hivi viongozi mnajua mnavyotamba timu zenu kupanda ndege mnajishusha thamani bila kujijua?

Zamani Majimaji waliwahi kutoka kwao Songea kuja Dar es Salaam kwa usafiri wa anga na hakikuonekana kitu kikubwa. Ilionekana kawaida. Kama watu wale wa Majimaji waliuchukulia kawaida usafiri wa anga, inakuwaje timu ya daraja la Simba na Yanga inafurahia kupanda ndege? Kuna tatizo sehemu kwenye soka letu! Si bure.

Timu za daraja la kwanza au Lipuli FC na Njombe Mji, zinaweza kujipiga kifua mitaani zikatamba na tukazielewa kama zingepata fursa ya kusafiri na anga kutokana na uchanga wao katika soka.

Lakini ni fedheha kwa Simba, Yanga kutumia usafiri huo na kutamba waziwazi kama walivyotamba viongozi wa Simba hivi karibuni. Ifike hatua maisha ya usafiri wa anga uonekane kawaida kwa timu hizo.

Ukubwa wa majina ya timu hizo wanaweza kumiliki ndege zao binafsi na mambo mengine makubwa ya kimaendeleo klabuni, lakini tuna viongozi wanaotazama zaidi leo yao kuliko kesho ya viongozi wengine, ndiyo maana usafiri wa anga imeonekana habari ya mjini.

Kiujumla Simba na Yanga haziishi kibiashara kama timu nyingine kubwa Afrika zinavyoishi katika mfumo huo. Zina mapungufu mengi ambayo kwa daraja lao ni fedheha, mwisho wa yote haishangazi kuona Simba wakishangailia kupanda ndege kwenda Mbeya.

Ndiyo maana maendeleo yao makubwa timu hizo ni kusemana na kuitana majina yasiyo na tija yoyote ile. Huyu anamtania mwenzie kwa kumuita Wamchangani, yule anamtania mwenzie kwa kumuita Wamatopeni. Hapa ndipo ulipogotea upeo wao wa ufikiri kwenye suala zima la kimaendeleo!

Katika dunia ya sasa ambayo soka si burudani pekee na imeshageuka kuwa biashara inayolipa vyema, tulipaswa kuona mabadiliko haya kwa timu zetu kubwa za nyumbani, lakini hazina maendeleo yoyote yale.

Sasa hivi tulitakiwa kusikia stori za Simba, Yanga zikizindua viwanja vyao vya mazoezi kwa timu zao za miaka 15 kushuka chini, huku tukisikia na stori nyingine za kuwapeleka Ulaya vijana wenye vipaji kwa ajili ya kufundishwa soka. Haya ndiyo maendeleo tunayopaswa kusikia watu wakijitamba nayo mitaani na mitandaoni. Dunia ya leo iko hivi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here