Home Habari SIMBA, YANGA ZAPEWA SIKU 75 KUKAMILISHA UCHAGUZI

SIMBA, YANGA ZAPEWA SIKU 75 KUKAMILISHA UCHAGUZI

7114
0
SHARE

NA EZEKIEL TENDWA

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limetoa siku 75 kwa klabu za Simba na Yanga kuhakikisha zinafanya uchaguzi wa kuwapata viongozi wapya.

Kwa mujibu wa Rais wa Shirikisho hilo, Wallace Karia, wameziandikia barua klabu hizo kuhakikisha zinatimiza agizo hilo ndani ya muda uliopangwa.

Alisema, Simba wanatakiwa kufanya uchaguzi baada ya uongozi uliopo madarakani kumaliza muda wao, huku Yanga wao wakitakiwa kuziba nafasi za viongozi walioachia ngazi.

“Tumetoa siku 75 kwa Simba kufanya uchaguzi lakini pia Yanga nao kujaza nafasi za baadhi ya viongozi wao ambao wamejiuzulu,” alisema.

Kuhusu Mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji, ambaye aliiandikia klabu hiyo barua ya kujiuzulu, Karia alisema mpaka sasa TFF wao wanamtambua kama ni kiongozi halali wa Wanajangwani hao.

“Sisi hatuna barua yoyote inayotuonyesha kwamba Manji ameachia ngazi Yanga, badala yake walituletea barua ikionyesha kuwa bado wao (Yanga) wanamtambua kama Mwenyekiti wao,” alisema.

Yanga wanatakiwa kujaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti baada ya Clement Sanga, kujiweka kando, Katibu Mkuu baada ya Charles Mkwasa naye kuachia ngazi pamoja na baadhi ya wajumbe.

Akizungumzia suala hilo, msemaji wa Yanga, Dismas Ten, alisema wanatambua changamoto iliyopo ya baadhi ya viongozi wao kujiuzulu na wao kwa kushirikiana na Bodi ya Wadhamini wanalishughulikia.

“Tunajua kwamba tunayo changamoto ya baadhi ya viongozi wetu kujiuzulu, lakini niwahakikishie mashabiki na wanachama wetu kuwa sisi Kamati ya Utendaji na Bodi ya Wadhamini, tutafanya kila liwezekanalo kuweka mambo sawa,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here