Home Habari SIMBA YASUBIRI MINOTI YA NDEMLA

SIMBA YASUBIRI MINOTI YA NDEMLA

2618
0
SHARE

SAADA SALIM NA EZEKIEL TENDWA

BAADA ya kiungo wa Simba, Said Ndemla kufuzu majaribio katika klabu ya AFC Eskilstuna ya Sweden, uongozi wa Wekundu hao wa Msimbazi upo katika mazungumzo kwa ajili ya kumuuza jumla.

Ndemla alikwenda nchini humo kwa ajili ya majaribio ya siku 14, ambapo alicheza nafasi ya kiungo kama kawaida wiki ya kwanza, lakini wiki ya mwisho alibadilishiwa namba akichezeshwa kama mshambuliaji na kuonyesha uwezo mkubwa.

Taarifa za uhakika kutoka Sweden zilizolifikia DIMBA, zinadai kwamba, benchi la ufundi la klabu hiyo limeridhika na uwezo wa Ndemla, ambapo kwa sasa wanafanya mazungumzo kwa ajili ya kupata huduma yake.

“Ukweli ni kwamba alifanya vizuri katika majaribio yake na hiyo timu inataka kufanya mazungumzo na Simba, ili kujua dau la kumchukua moja kwa moja,” alisema rafiki wa karibu wa Ndemla.

DIMBA lilimtafuta Katibu Mkuu wa Simba, Arnold Kashembe, ambaye alisema kwa upande wao bado hawajapata taarifa rasmi, lakini kama amefuzu majaribio uongozi unampongeza na utakuwa tayari kuzungumza na klabu husika.

“Hatujapata taarifa rasmi za kwamba amefuzu, lakini kama ni hivyo niseme haitushangazi, kwani Ndemla ni mmoja wa vijana wanaojituma sana, ngoja tusubiri huko, wakija sisi tutakuwa tayari kumuuza, kwani tulimruhusu kwa moyo mmoja kwenda kufanya majaribio,” alisema.

Hata hivyo, jana jioni wakati tunakwenda mitamboni, uongozi wa Simba kupitia kwa Ofisa Habari wake, Haji Manara, ulithibitisha kupitia taarifa rasmi ya klabu kuwa, mchezaji huyo amefuzu majaribio.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here