Home Habari SIMBA YAWEKA WAZI USAJILI WAKE

SIMBA YAWEKA WAZI USAJILI WAKE

1869
0
SHARE

NA SAADA SALIM


 

SIMBA wameamua kufanya mambo yao kimya kimya katika kuhakikisha wanaboresha zaidi timu yao kwa kufanya usajili kulingana na mapendekezo yaliyotolewa na kocha wao, Joseph Omog.

Wakati Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo ilipokutana na kuijadili ripoti ya kocha wao huyo, alichopendekeza ni usajili wa wachezaji watatu pekee.

Wachezaji ambao amewataka Omog ni kipa ambapo sasa wanaotajwa ni kipa wa Azam FC, Aishi Manula na yule wa African Lyon, Youthe Rostand, huku pia klabu hiyo ikitarajiwa kuziba nafasi ya beki wa kati pamoja na mshambuliaji wa kati mmoja.

Katika kikao hicho cha Kamati ya Utendaji iliyokutana wiki iliyopita, majina ya Manula na Rostand inasemekana yalijadiliwa kwa muda mrefu na kwamba huenda mmoja kati yao akasajiliwa kumsaidia kipa wa sasa, Vincent Angban.

Taarifa zaidi kutoka Simba zinadai kuwa, kuna ugumu wa kumpata Manula, kutokana na kuwa na mkataba na Azam FC, lakini kwa upande wa Rostand yeye ameweka wazi kuwa klabu inayomtaka iwe tayari kuweka mezani kitita cha Sh milioni 30 za Tanzania, ndipo akubali kumwaga wino na kuvaa uzi mwekundu.

Kamati hiyo ya utendaji na ile ya usajili wamefikia hatua ya kumpendekeza Manula na Rostand, kwani taarifa zinadai kuwa, Omog hakutaja jina lolote na badala yake amewaambia wao waangalie tu atakayefaa.

DIMBA Jumatano lilimtafuta Omog ili kuzungumzia suala hilo, ambapo alisema kwa sasa yupo kwao Cameroon kwa ajili ya mapumziko ya muda mafupi, huku akisisitiza kila kitu amewaachia viongozi.

“Sitakuwa na mabadiliko makubwa katika timu yangu, ninachokiangalia zaidi ni kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza mzunguko wa kwanza, ninachoweza kukuambia ni kwamba, nilishakabidhi ripoti yangu kwa uongozi na ninaamini wataifanyia kazi vizuri,”  alisema.

Taarifa zaidi zinadai kuwa, awali kulikuwa na tetesi za wekundu hao wa Msimbazi kukata wachezaji wengi, lakini sasa wameamua kutokufanya mabadiliko makubwa, kwani yanaweza kuwaathiri mbele ya safari.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here