SHARE

NA FARAJA MASINDE

LICHA ya kwamba kwa sasa siyo tena Kocha wa Machester United, lakini bado jina na heshima yake kwa wapenzi na mashabiki wa soka ulimwenguni vipo, ambapo wanamuona kama mwalimu bora wa mpira kuwahi kutokea katika klabu yao kutokana na mafanikio aliyoyaacha.

Huyu ni kocha mstaafu wa klabu ya Manchester United, Sir Alex Ferguson, ambaye aliwahi kusema kuwa mchezo wa mpira wa miguu utakuwa bora na wa kuvutia zaidi ulimwenguni iwapo teknolojia zaidi itatambulishwa michezoni.

Ferguson aliwahi kutoa mtazamo wake huo wakati akisifia teknolojia ya Goal-line kama moja ya teknolojia bora na kubwa kuwahi kuwapo michezoni ambayo ilianza misimu kadhaa iliyopita katika Ligi Kuu ya England.

Teknolojia hiyo imekuwa na msaada mkubwa zaidi kwa waamuzi pindi wawapo uwanjani.
Itakumbukwa kuwa, Ferguson ni mmoja wa makocha ambao walikuwa wakiwanyooshea kidole waamuzi kwa kiwango kikubwa sana kutokana na kile kilichokuwa kinaelezwa kuwa alikuwa hafurahishwi na maamuzi yao pindi wanapokuwa uwanjani.

Anasema ni jambo la faraja kuona kuwa ulimwengu huu wa teknolojia umekuwa na faida hata kwenye nyanja ya michezo, jambo lililofanya mambo mengi kuendeshwa kwa uwazi zaidi.

“Teknolojia itaongeza uwazi zaidi michezoni, watu kama waamuzi hawana kazi kubwa ya kufanya siku hizi. Hii ni kutokana na kazi kubwa inayofanywa na teknolojia hii ya Goal-line, kwani huwezi kubishana na teknolojia hii pindi inapoeleza tukio husika.

“Teknolojia ya Goal-line ni nzuri sana, ngoja tuendelee kuipa nafasi na kuisambaza zaidi kwenye maeneo mbalimbali, kwani ni mfumo ambao umeleta tofauti kubwa sana kwenye ulimwengu huu wa soka,” anasema Ferguson.

HISTORIA YAKE
Ferguson ni mzaliwa wa Scotland ambaye amefanikiwa kucheza soka kwa mafanikio makubwa zaidi mpaka kufikia hatua ya kuwa Meneja wa klabu yenye mvuto zaidi duniani ya Manchester United, huku akiwa ni meneja aliyedumu kwa muda mrefu zaidi.

WASIFU
Ferguson alizaliwa Desemba 31, 1941 katika mji wa Glasgow, Scotland na jina lake lilianza kuwa kubwa katika medani ya soka baada ya kuanza kucheza mpira katika timu ya Dunfermline Athletic.
Baadaye alijiunga na timu ya Aberdeen FC kama Meneja kuanzia mwaka 1986 na baadaye kujiunga na klabu ya Manchester United na kuifanya kushinda mataji mengi kwenye soka la Ulaya.

Alexander Chapman Ferguson alizaliwa kwa wazazi wawili ambao ni Alexander Sr na Elizabeth katika mji wa Glasgow, Scotland.

MEDANI YA SOKA
Katika mwaka 1967, Ferguson alijiunga na klabu ya Glasgow, Rangers F.C, uhamisho ambao ulivunja rekodi nchini Scotland, kwani uligharimu dola 179,000, sawa na pauni 65,000, hata hivyo, mwisho wake haukuwa mzuri kwenye klabu hiyo.

UMENEJA
Ferguson alianza umeneja mwaka 1974 katika klabu ya East Stirlingshire na hivyo kuleta ushindani mkubwa.
Ferguson alikabidhiwa mikoba ya Man United Novemba, 1986, ambapo alifanya vyema kwenye msimu wa 1989-90, mpaka kufanikiwa kuchukua taji la FA mwaka huo huo.
Hakuishia hapo, mwaka uliofuata alitwaa taji la Ulaya na baadaye kutwaa lile la ligi mwaka 1992 na kufuatiwa na la ligi kuu ya Uingereza 1993.

Mafanikio zaidi ya Ferguson yalikuja msimu wa 998/1999, baada ya kuwa kocha wa kwanza wa Uingereza kushinda mataji matatu mfululizo ambayo ni, Ligi Kuu, FA na UEFA.
Mwaka 2003, Ferguson alipokea tuzo ya kocha bora wa kipindi cha miaka 10 mfululizo katika Ligi Kuu ya England.

Kifupi Ferguson ambaye alitangaza kuachana na ukufunzi wa soka Mei 8, 2013, ameipatia Man United mataji 19 ya Ligi Kuu ya England, huku akiipa timu hiyo jumla ya mataji 38 kwa kipindi cha miaka 27 aliyoitumikia kama mwalimu.

MAISHA BINAFSI
Ferguson alioana na Cathy Holding mwaka 1966, ambaye wamejaliwa kupata watoto watatu wa kiume: Mark, Darren na Jason.
Darren aliwahi kucheza muda mfupi sana katika klabu ya baba yake, Manchester United miaka ya 1990 na kisha baadaye akawa kocha.
Furguson, ambaye ni mfuasi wa siku nyingi wa chama cha Labour, pia aliwahi kuhudumu kama balozi wa UNICEF Uingereza.
Baada ya kukabidhiwa mikoba katika klabu ya Manchester aliandika historia mwaka 1999, baada ya kuzawadiwa tuzo ya heshima katika siku ya heshima ya kuzaliwa kwa Malikia.

Kocha huyo bora kabisa kuwahi kutokea duniani na ambaye mfupa wake mpaka sasa unatajwa kukosa mtu wa kuutafuna vyema pale Man United, anakadiriwa kuwa na utajiri wa dola milioni 50, ambapo inaaminika kuwa mwaka wake wa mwisho alikusanya pauni milioni 34.

Ferguson, ambaye ni babu wa wajukuu 11, aliwahi kutangaza kuwa atatumia sehemu ya muda wake kuwa mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Harvard katika kozi mpya inayofahamika kama The Business of Entertainment Media & Sports, huku Agosti mwaka jana, akiingiza sokoni kitabu chake cha Leading.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here