SHARE

NA NIHZRATH NTANI

       Katika ulimwengu wa soka Duniani, kuna ligi kubwa mbili ambazo zimepelekea kuwa na upinzani mkubwa unaoletwa na mashabiki wanaofuatilia ligi hizo. Kila kukicha ,kumekuwepo na mijadala mbalimbali kutoka kwa mashabiki wa soka Duniani .

Mijadala yao ,mara nyingi huwa inashindwa kutoa hitimisho sahihi miongoni mwa wapenzi ,kwa kila mmoja kutetea upande wake kwa hoja wanazoziamini kuwa ni sahihi na kubaki kuendelea kukinzana.

LA LIGA VS EPL

Ni ligi kuu ya England maarufu kwa jina la EPL na ile ligi kuu ya Hispania inayojulikana kwa jina la La Liga. Ndizo ligi zinazoongoza kufuatiliwa na wapenzi wengi wa soka Duniani.

Mashabiki wengi wamegawanyika kwa pande mbili ,na kupelekea mapenzi yao kwa vilabu mbalimbali vinavyoshiriki ligi mojawapo kutoka katika nchi za England na Hispania.

Bila shaka ,EPL ni ligi maarufu sana Duniani kuliko La Liga na ndio inayoongoza kufuatiliwa na mashabiki kote ulimwenguni ,kutokana na sababu kadhaa ikiwamo za kiuchumi.

Taifa la England inachukuliwa kuwa ni miongoni mwa Taifa tajiri Duniani likiwa Taifa la pili kuwa na vyombo vingi vya habari ambavyo vinasaidia kuitangaza ligi yao tofauti na Hispania. Pia ,sababu ya lugha ya kiingereza imeifanya ligi kuu ya England kufuatiliwa sana kwa kuwa ya lugha ya kiingereza ndio inayoonekana kama lugha kuu ya mawasiliano ya kimataifa.

Lakini pamoja na mapenzi yao ya ushabiki wa vilabu vya Uingereza bado mashabiki hawa wamekuwa wakionesha mapenzi yao kwa vilabu vya Real Madrid na Barcelona kutokana na sababu mbalimbali zinazowapelekea wavutiwe kushabikia vilabu hivyo viwili vya Hispania.

Bila shaka ,wana haki ya kufanya hivyo ikizingatiwa vilabu vya Barcelona na Real Madrid ndizo klabu zinazochukuliwa kuwa klabu kubwa kuliko zote Duniani. Klabu ambazo wachezaji bora na mahiri kabisa wamewahi kuzichezea na wengine wakibakia na ndoto zao za siku moja kuvaa jezi za klabu hizo.

Katika ligi kuu ya England , klabu za Manchester United, Liverpool, Tottenham, Arsenal na Chelsea, ndizo zinachukuliwa kuwa zina wapenzi wengi wanaoziunga mkono.

Hata hivyo, pamoja na kuwa na mapenzi na timu hizo bado mashabiki hao wamekuwa na mapenzi na vilabu vya Hispania hasa vilabu vya Real Madrid na Barcelona na hawawezi kuficha hisia zao pale ambapo michezo ya timu hizo zinapochezwa ama wanapokutana wenyewe kwa wenyewe katika ile mechi yao maarufu ya El Clasico. Hapo ndipo utapata kuwafahamu zaidi.

MASHABIKI WA MANCHESTER UNITED KUIPENDA REALMADRID

Klabu ya Manchester United inasemekana ndio inayoongoza kwa kuwa na mashabiki wengi Duniani kwa sasa. Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti za kiutafiti zinaeleza asilimia 95 ya mashabiki wa timu hii wengi wao wanavutiwa kuipenda Real Madrid .

Kuna maelezo kuwa kuna sababu ya kihistoria katika ya vilabu hivi viwili tangu enzi na enzi. Lakini pia ,hatua ya Real Madrid kuwa na tabia ya kusajili wachezaji wao nyota wa Manchester United, imesaidia kuongeza mahaba kwa mashabiki wa Manchester United kwa Real Madrid.

Uhamisho walioufanya wa Cristiano Ronaldo klabuni Real Madrid kutoka Manchester United ukaifanya klabu hiyo kuzoa mashabiki lukuki wa Manchester United. Ronaldo bado anaendelea kubaki katika mioyo ya mashabiki wengi wa Manchester United hasa baada ya kuisaidia klabu hiyo kutwaa mataji mengi likiwemo taji la mabingwa wa Ulaya mwaka 2008.

Wakati wanapoitazama La Liga katika mechi za Barcelona na Real Madrid asilimia kubwa ya mashabiki wa Manchester United huiunga mkono Real Madrid kwa sababu ya unasaba wao.

Hali hiyo inawafanya mashabiki wa Manchester United kuichukulia Real Madrid kuwa timu yao baada ya Manchester United.

MASHABIKI WA ARSENAL KUIPENDA FC BARCELONA

Wakati linapokuja suala la Barcelona na Real Madrid, mjadala wao huwa mkubwa. Kwa sababu, ni zaidi ya muongo mmoja, tumeshuhudia kila linapofikia msimu wa usajili kukiibuka ushindani kati ya timu hizi mbili.

Ambao hushindana kununua wachezaji nyota kutoka katika vilabu vya England. Real Madrid wao huvamia klabuni Manchester United wakati wapinzani wao huenda kuvamia klabuni Arsenal.

Ni wachezaji nane mpaka sasa wameweza kuhama kutoka Arsenal kwenda Barcelona tangu zama za Emmanuel Petit na Marc Overmars kisha nyakati za Aleksander Hleb na Alex Song huku wa mwisho ni Thomas Vermalen.

Wachezaji hawa wote walikuwa vipenzi vya mashabiki wa Arsenal na kuhama kwao kukapelekea mashabiki wengi wa Arsenal kujikuta wakihamisha mapenzi yao kwa Barcelona. Pia, kufanana kwa staili ya soka lako ni jambo lililowavutia sana mashabiki wa Arsenal kuipenda Barcelona.

UPINZANI WA ARSENAL VS MANCHESTER UNITED

 Upinzani wa Arsenal na Manchester United ndani ya Ligi kuu ya England umepelekea kuhamisha upinzani wao hadi ligi kuu ya Hispania na kujikuta wakienda tofauti katika mapenzi yao.

Mashabiki wa Arsenal na Manchester United katu hawawezi kushabikia timu moja hivyo, wale wa Arsenal wako Barcelona na wale wa Manchester United wako Real Madrid.

Ni nadra sana kuona shabiki wa Manchester United akiichukia Real Madrid na Shabiki wa Arsenal kuichukia Barcelona kutokana na historia za timu hizo.

MASHABIKI WA CHELSEA, LIVERPOOL NA TOTTENHAM WAGAWANYIKA.

Wakati huu ambapo Liverpool wakiwa wamerejea kiushindani ni nadra kuwaona mashabiki halisi wa klabu hii wenye umri wa ujana.

Na wengi wanabakia wale wenye umri wa makamo .Hata hivyo, mashabiki wachache wa timu hii wamegawanyika katika mapenzi yao kwa timu za Real Madrid na Barcelona.

Zamani asilimia kubwa ya mashabiki wa klabu hii walikuwa wanaiunga mkono Real Madrid hasa uwepo wa wachezaji wao waliokuwa vipenzi vyao kama Steve Mcmanaman, Michael Owen, Jerzy Dudek, Alvaro Arbeloa na Xabi Alonso, lakini kwa wakati huu mashabiki wengi wa Liverpool wamekuwa wakiiunga mkono klabu ya Barcelona hasa baada ya uhamisho wa Luis Suarez aliyekuwa mchezaji wao nyota Liverpool.

Mashabiki wa Tottenham Hospurs wao wanaendelea kuvaa jezi za Real Madrid katika mitaa yote ya kaskazini mwa jiji la London. Huku wakijivunia wachezaji wao nyota waliokuwa vipenzi vyao klabuni Spurs. Uwepo wa Gareth Bale na Luca Modric klabuni Real Madrid.

Limekuwa jambo lililowavutia mashabiki wengi wa Spurs kuipenda Real Madrid na kuanza kuifuatilia. Wakati huo huo uwekezaji mkubwa uliofanywa na tajiri wa kirusi Roman Abramovic klabuni Chelsea umepelekea klabu hiyo kupata mashabiki wengi vijana ambao wameanza kuipenda timu hiyo.

Hata hivyo, mashabiki hao pamoja na kuipenda Chelsea bado wamekuwa na mapenzi makubwa na vilabu vya Hispania vya Real Madrid na Barcelona. Huku asilimia 70 za mashabiki wa Chelsea wanatajwa kuwa na mapenzi na klabu ya Barcelona huku asilimia 30 wakiwa na mapenzi na klabu ya Real Madrid kabla ya uhamisho wa Eden Hazard kwenda Real Madrid.

Upepo unaweza kugeuka msimu huu baada ya uhamisho huo kwa mashabiki wa chelsea kuanza kuipenda Real Madrid.

Pamoja na yote, hakuna ubishi kuwa vilabu vya Barcelona na Real Madrid ndiyo vilabu maarufu zaidi Duniani na mashabiki wengi wa soka wamegawanyika katika pande mbili kwa klabu hizi.

Umaarufu wa timu hizi mbili hujikuta wakikusanya wachezaji nyota na wa daraja la juu. Na hakuna timu yoyote kutoka England inayoweza kuleta ushindani na timu hizi katika soko la usajili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here