SHARE

NA SAADA SALIM,

BAADA ya kumwagiwa fedha lukuki kutoka sehemu mbalimbali, beki kisiki wa Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, ameweka wazi siri inayomfanya kuwavutia mashabiki wengi.

Tshabalala amefanikiwa kuwa kipenzi cha mashabiki wa soka nchini kutokana na uwezo mkubwa anaouonyesha katika kikosi chake cha Simba pamoja na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, hali iliyowafanya baadhi yao kummwagia fedha.

Katika futari ya Simba iliyoandaliwa na uongozi mwishoni mwa wiki iliyopita, na kufanyika katika Hoteli ya Serena, mashabiki wengi walimpa fedha baada ya kutangazwa kuwa mchezaji bora wa msimu kwa upande wa Simba.

Mbali na hiyo, pia Tshabalala alizoa fedha nyingine baada ya kuibuka mchezaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara, hayo yakiwa mafanikio yake makubwa ndani ya soka la Tanzania.

Pia Tshabalala alipokea kitita cha Sh 500,000, kutoka kwa kampuni ya mafuta ya Big Bon, ambapo beki huyo ameliambia DIMBA Jumatano kuwa, siri ya mafanikio hayo ni kutokana na kujituma na ushirikiano anaoupata kutoka kwa wachezaji wenzake, benchi la ufundi pamoja na mashabiki kwa ujumla.

“Siwezi kusema mengi sana, lakini kwa ujumla mafanikio hayo yanatokana na kujituma, kushirikiana na wachezaji wenzangu, sapoti ya uongozi na mashabiki, naamini peke yangu nisingeweza kufika hapa nilipofika, ila kwa ushirikiano,” alisema beki huyo, ambaye kwa sasa anauguza majeraha ya mguu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here