SHARE

MANCHESTER, England

KAMA ulidhani Manchester United wanaweza kufanya miujiza yoyote msimu huu, sahau hilo. Kocha wa timu hiyo, Ole Gunnar Solskjaer amewataka mashabiki wa mabingwa hao wa zamani wa England kuwa wavumilivu, kwani anajenga kikosi ili kije kutisha miaka ijayo.

Solskjaer raia wa Norway alisema ni ngumu kuahidi mafanikio katika kikosi hicho, sababu bado kuna mambo bado hayajakaa sawa huku akidokeza kuwa hata ule ubabe wao wa zamani inabidi mashabiki wasahau.

Aliendelea kusema ili warejee kwenye yale mafanikio waliyokuwa nayo miaka ya 1990, yanatakiwa kujengwa kupitia kikosi hiki kilichozungukwa na wachezaji wengi chipukizi wenye kuanzia umri wa miaka 18.

Kocha huyo ni wanne tangu Sir Alex Ferguson aondoke Manchester United lakini hakuna mafanikio yoyote ambayo yamepatikana zaidi ya kuendelea kushuka.

“Hatupo miaka ya 1990, hiki ni kipindi tofauti ambacho tunahitaji uvumilivu ili kujenga timu upya, tunajua kutakuwa na vikwazo na mafaniko lakini malengo yetu bado yapo hai.

“Nipo tayari kuirudisha Manchester United katika ubora wake, lakini lazima tuweke msingi mzuri ambao utaanzia kwa vijana na timu itakuwa ya muda mrefu.

“Hakuna timu ambayo ina utamaduni wa kutoa nafasi kwa wachezaji chipukizi kama sisi, tutaendelea kufanya hivyo sababu hilo ni sehemu ya maisha ya hapa.

“Mashabiki inabidi waelewe hata mimi na benchi langu tunaposhindwa kupata matokeo ya ushindi huwa tunasononeka lakini hatukati tamaa sababu tunajua huu ni mchakato wa muda mrefu,” alisema.

Juzi, Manchester United walishinda mabao 2-0 dhidi ya Chelsea katika mchezo wa Ligi Kuu England uliochezwa Uwanja wa Stamford Bridge.

Pia, Solskjaer anaamini kikosi chake kitafanikiwa kufanya vizuri msimu huu kwa kumaliza ndani ya timu nne za juu ‘top four’ huku akijipa matumaini ya kutwaa taji la Ligi ya Europa.

Kesho, Manchester United watakuwa wageni wa Club Brugge ya Ubelgiji katika mchezo wa hatua ya 32 bora ya Europa, kisha wikiendi watacheza mechi nyingine ya Ligi Kuu dhidi ya Watford ndani ya Uwanja wa Old Trafford.

“Haijalishi ukubwa au udogo wa kikombe, Manchester United ni timu inayotakiwa kushinda kila kitu inachopigania sababu ni utamaduni wa klabu hii, tutapambana kwenye ligi na kuangalia uwezekano wa kushinda taji la Europa msimu huu,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here