SHARE
Heung-Min Son

LONDON, England

MAJANGA. Kikosi cha Tottenham kimeendelea kuandamwa na majeruhi baada ya taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo kusema winga Heung-Min Son atafanyiwa upasuaji baada ya kuvunjika mkono dhidi ya Aston Villa, wikiendi iliyopita.

Son raia wa Korea Kusini aliumia mkono wa kulia dakika za mwanzo baada ya kugongana na beki wa Aston Villa, Ezri Konsa, endapo upasuaji huo ukikamilika, winga huyo atakuwa nje kwa wiki zisizopungua tatu.

Hata hivyo, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 alimaliza mchezo huo na kufunga mabao mawili kati ya matatu yaliyopeleka ushindi kwa Tottenham.

“Son atafanyiwa upasuaji wiki hii baada ya kuvunjika mkono wake wa kulia, aliumia dhidi ya Aston villa, kila kitu kikikamilika kitengo chetu cha matibabu kitasimamia uponaji wake na atakuwa nje kwa wiki kadhaa,” ilisema taarifa iliyotolewa na Tottenham.

Son alikuwa mchezaji wa kutegemewa wa klabu hiyo yenye maskani yake London tangu alipoumia straika Harry Kane, Mkorea huyo amefunga mabao sita katika michezo mitano ya karibuni. Pia, amefunga mabao 16 kwenye michuano yote msimu huu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here