SHARE

NA ALLY KAMWE,

MIMI ni miongoni mwa watu wachache sana duniani tunaoichukia demokrasia, unajua kwanini? Mwanafalsafa wa Kigiriki, Plato ana jibu sahihi.

Siku moja katika masiku mengi ya maisha yake aliyowahi kuishi duniani, Plato alisema: “Tatizo pekee la demokrasia, hata mjinga ana haki ya kusema na akasikilizwa.”

Ndiyo, ni demokrasia pekee inayoamini kwenye wingi na si hoja.

Mara zote mjinga husema kwa sababu anataka kusema, lakini mwerevu husema pindi anapokuwa na sababu  ya kusema.

Ni demokrasia iliyompa uhuru leo hii El Hadji Diouf kusema aliyotaka kusema kwa Steven Gerrard, tuna cha kumfanya? Hatuna, njia rahisi kwetu ni kumsikiliza na kumpuuza tu.

Imekuwa wiki ngumu kwa wapenzi wa soka duniani, habari za Steven Gerrard kustaafu soka zimeacha simanzi kubwa kwenye mioyo yetu, tulijua angestaafu, lakini hakuna aliyejiandaa kuliona hilo likitokea kwa sasa.

Leo hii, taarifa yoyote ya Andre Pirlo kustaafu soka itakuja tukiwa na  mengi ya kumwambia, tumeshajiandaa kumuaga kama ambavyo tumeandaa maua ya kumpa Fransesco Totti.

Gerrard, kwa ugumu wa viungo mpaka moyo aliobarikiwa kuwa nao, hakuna aliyetegemea safari yake ya soka ingemalizika akiwa na miaka 36. Ametushtua sana!

Wengi wamesikitika, kila aliyebora kwenye ulimwengu wa soka amezungumza kwa namna bora jinsi anavyofahamu ubora wa Steven Gerrard. Umesikia kauli ya Thiery Henry?

Moja katika majuto yake makubwa kwenye soka ni kutocheza pamoja na Steven Gerrard.

Haijatosha kwake kucheza na Lionel Messi au Andres Iniesta, kumkosa Gerrard anaamini amekosa kitu kikubwa kwenye maisha yake.

Lakini kwa bahati mbaya zaidi, siku ambayo Gerrard ameketi chumbani akisoma jumbe za hongera kutoka sehemu mbalimbali duniani, anaibuka El Hadji Diouf.

Huyu hamkubali kabisa Steven Gerrard. Kuna sehemu katika moyo wake ina chuki dhidi yake, anaishi amkichukia siku zote. Hajawahi kumpenda hata kwa bahati mbaya.

Ni sawa, hata mwendawazimu ana moyo wake wa kupenda.

Diouf ameamua kumchukia Gerrard na ni vyema kama angeendelea kumchukia kwa sababu zake za kibinadamu na kuacha kuzungumza jambo lolote la Gerrard ndani ya uwanja.

Hili la kusema Gerrard si lolote na wala hajafanya lolote la maana kwenye mchezo wa soka, Diouf amejikosea na ametukosea sana.

Na hii inaweza kuwa laana yake ya pili duniani, baada ya ile aliyopewa na Gerald Houllier kipindi kile? Unaijua ni laana ipi? Tulia nitakwambia.

Nimesikia hoja zake kwanini anaamini Gerrard si lolote kwenye ramani ya soka, ni wazi alitenga muda wa kuziandaa na zikawa na mpangilio mzuri usioeleweka.

Moja, Diouf anasema Gerrard alikuwa akimuonea wivu kwa mafanikio yake aliyoyapata akiwa na Senegal. Mafanikio yapi? Kucheza robo fainali kwenye kombe la dunia. Kweli?

Kwa haraka haraka, hoja hii inasikika vyema masikioni.

Kila mwanadamu ana madhaifu yake, lakini kwa kuamini kuwa Gerrard alikuwa anawaza kitu kikubwa kwa England kuliko Liverpool ni mawazo ya mwanadamu aliyechoka kufikiri.

Kweli Senegal walicheza robo fainali ya kombe la dunia, hatua ambayo Gerrard hajawahi kucheza akiwa na England, lakini unaamini moyo wa Gerrard una sikitiko lolote juu ya hilo?

Angekuwa na chuki ya namna gani kwa Fernando Torres? Hapa Diouf afikirie upya.

Steven Gerrard yuko mmoja tu duniani, yule mwanamume aliyevuja jasho na damu kwa ajili ya Liverpool.

Pili Diouf anajaribu kutaka kuiaminisha dunia kuwa Gerrard anapenda kutukuzwa na kuwa mfalme pekee wa Liverpool, yeyote atakayejaribu kuzima nyota hiyo, hupishana naye.

Hapa alichosahau Diouf ni kuwa ufalme wa Gerrard pale Anfield haukuja kwa sababu alianza soka lake pale, haukuja tu kwa kuwa alipenda kuwa.

Ufalme wa Gerrard ulitokana na malipo ya jasho alilovuja kwa miaka 19 pale ‘Merseyside’. Amepambana kiume kuifanya Liverpool kuwa timu ya kiume unayoiona leo hii duniani.

Pamoja na ubora wa miguu ya Diouf, bado hakuwa mchezaji mwenye moyo wa kucheza Liverpool. Akili yake iliwaza mambo mengi nje ya uwanja kuliko matokeo ya ndani ya uwanja.

Timu ingefungwa mchezo muhimu na bado angetoka na kurudi kwenye gari na kufungulia muziki kwa sauti ya juu, wapi mwanadamu wa aina hii anaweza kuishi kwenye moyo wa ‘simba’ kama alionao Gerrard?

Lile tukio la kumtemea mate shabiki wa Celtic linabaki kuwa tukio la aibu zaidi kufanywa na mchezaji wa Liverpool.

Mbali na kuharibu wasifu wake, liliharibu pia heshima ya klabu, ni mtu huyu leo anayesimama na kujitamba kuwa anamchukia Gerrard, acha demokrasia iwe demokrasia!

Diouf kabla hajanyoosha kidole chake kimoja kwa Gerrard anatakiwa afanye tathmini ya vidole vitatu vilivyonyooka kifuani kwake, kaifanyia nini cha maana Liverpool?

Mtu aliyefunga mabao 6 kwenye mechi 82 alizocheza kwenye eneo la ushambuliaji ana lipi la maana alilofanya mbele ya mtu aliyefunga mabao 186 akiwa na jukumu la kucheza katikati ya uwanja?

Nilicheka sana pale Diouf alipojitapa kuwa jina lake lipo kwenye orodha ya wachezaji 100 bora duniani waliotajwa na Pele.

Kwa akili ya kawaida kabisa, unafikiri Gerrard atakuwa na sababu ya kujilaumu au kuona aibu kutokuwemo kwenye orodha ile ikiwa Lionel Messi na Cristiano Ronaldo hawapo?

Pele abaki na orodha yake na ulimwengu wa soka tubaki na orodha yetu, Gerrard anabaki kuwa bora katika bora waliowahi kuishi kwenye ramani ya soka duniani.

Mwambieni Diouf, asichoweza kufanya, hawezi kukizungumza. Kama alishindwa kupata heshima Liverpool kwa miguu yake, asitegemee kuipata sasa kwa mdomo wake!

Kila la heri ‘Captain Fantastic’, usiku wa Mei 25, 2005 pale Istanbul unabaki kuwa usiku bora kwenye maisha yangu ya kupenda soka duniani. Mzee wangu Kamwe General amenituma nikwambie ‘havache kwa vyothe’.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here