SHARE

TUNACHOTAKIWA kuomba Watanzania kwa imani zetu ni ushindi kwa timu ya Taifa Tanzania (Taifa Stars) dhidi ya Burundi katika mchezo utakaopigwa hii leo Jijini Bunjumbura.


Ni mchezo wa ugenini ambao Stars inapigania ushindi ili iweze kufuzu kupangwa kwenye makundi yatakayocheza fainali za Kombe la Dunia mwaka 2022, zitakazochezwa Qatar.


Baada ya mchezo huo, Stars itarejea nyumbani na kuwasubiri Warundi hao katika mchezo wa marudiano utakaopigwa Septemba 8, katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.


Tofauti na michezo mingi ambayo timu hiyo ilishiriki, safari hii hamasa ya Watanzania imeongezeka kiasi cha makundi mbalimbali ya mashabiki kutinga mapema, nchini Burundi kwa ajili ya kuwapa hamasa wachezaji.
Ukiacha mashabiki waliofurika kwa wingi vilevile benchi la ufundi la timu hiyo, chini ya kocha Etiene Ndayiragije limetoa neno la faraja kwa Watazania kwamba, kikosi chao kinaweza kuibuka na ushindi mnono.


Na sisi Dimba pia tunaungana na maelfu ya Watanzania kuiombea ushindi timu yetu hiyo ili iweze kusonga mbele.
Tuna imani kubwa na kikosi hiki cha Ndayiragije, hasa kutokana na kuita wachezaji wenye umri tofauti ili kupata mchanganyiko utakaoweza kuleta tija kikosini.


Imani yetu ni ushindi kwa Stars, hasa tukichukulia wapinzani wetu Burundi ambao kimsingi soka letu na lao linashabihiana na vilevile kuwepo kwa kocha anayeitambua timu hiyo bila shaka wachezaji watapata siri nyingi zitakazoweza kuchagiza ushindi.


Tunawaombea afya njema wachezaji, viongozi pamoja na mashabiki wanaotuwakilisha nchini Burundi ili waweze kutekeleza majukumu yao na hatimaye kutuletea ushindi Watanzania.


Dimba tunaamini umoja huu unaozidi kuongezeka na hamasa kubwa kwa Watanzania dhidi ya timu ya Taifa utaweza kutufikisha mbali katika medani ya soka ambayo miaka yote tumekuwa tukiipigania bila mafanikio. Mungu Ibariki Stars.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here