Home Habari STARS YANOGA BILA SAMATTA

STARS YANOGA BILA SAMATTA

294
0
SHARE

NA SALMA MPELI,

IKICHEZA bila straika wake ambaye pia ni nahodha Mbwana Samatta, timu ya soka ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ jana iliendelea kuwafurahisha mashabiki wake baada ya kuifumua Burundi kwa mabao 2-1.

Katika mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Stars ilikwenda mapumziko ikiongoza kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na Simon Msuva, huku lile la pili likifungwa kipindi cha pili na kinda wa Kagera Sugar Mbaraka Abeid.

Huo ulikuwa ni mchezo wa pili wa kirafiki chini ya kocha Salum Mayanga, aliyechukua mikoba ya Charles Boniface Mkwasa, ambapo katika mchezo wa kwanza dhidi ya Botswana mwishoni mwa wiki iliyopita waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 yote yakifungwa na Samatta.

Katika mchezo wa jana, Samatta hakuwepo kutokana na majukumu yaliyokuwa yanayomkabiri katika timu yake ya KRC Genk.

Stars ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 20 kupitia kwa winga wake Msuva ambaye aliitendea haki pasi ya mshambuliaji Ibrahim Ajib.

Lakini Dakika 54 Laudit Mavugo aliisawazishia Burundi bao la kusawazisha kwa mpira wa mbali baada ya kipa wa Stars Deogratias Munishi ‘Dida’ kutoka langoni.

Pongezi zimuendee Mbaraka Yusuf Abeid aliyechukua nafasi ya Farid Mussa, ambaye aliingia na kuipatia Stars bao la pili dakika ya 77, baada ya kupokea pasi kutoka kwa Ajib.

Baada ya kupokea pasi hiyo, staraika huyo aliuvuta kidogo mpira hadi ndani ya boksi kabla ya kufumua shuti lililogonga mwamba na kurudi, akauwahi na kufunga bao zuri.

Mchezaji huyo aliyeibukia kikosi cha pili cha Simba, jana alikuwa anchezea mechi ya kwanza Stars baada ya kuitwa na kocha Mayanga wiki iliyopita, lakini akacheza vizuri.

Kwa ujumla timu zote mbili zilionyesha kandanda safi dakika zote 90, japo washambuliaji wa timu zote mbili walishindwa kutumia vizuri nafasi walizokuwa wanatengenezewa.

Katika mchezo huo Stars iliwakilishwa na Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Abdi Banda, Salim Mbonde, Himid Mao, Simon Msuva, Mzamiru Yassin/ Jonas Mkude , Salum Abubakar/ Said Ndemla, Ibrahim Ajib Shiza Kichuya, Farid Mussa/ Mbaraka Abeid .

Burundi:  Duhayindaya Gael Nahimana, Jonathan Hererimana Rashid, Moussa Omary Nshimirimana David, Ndayishimiye Youssouf, Ndikumana Tresor, Ndarusanze Jean, Laudit Mavugo, Kiza Fataki na Nzeyimana Djuma.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here