SHARE

NA ABDUL MKENYENGE

KITU rahisi unachoweza kufundishwa na watu waliofanikiwa ni kujikubali, kuwa na imani na wewe mwenyewe kwanza. Kupenda unachofanya na kukithamini.

Kuamini hata kama hakuna anayekufata nyuma haimaanishi njia uliyochagua kupita si sahihi. Kila mtu ni shujaa wa maisha yake mwenyewe.

Miezi kadhaa iliyopita nilifanikiwa kusoma simulizi fupi ya maisha ya Mfalme wa Manchester United, Eric Cantona alichokiita kwa jina la ‘What is the meaning of life?’ akiwa na maana kwamba ‘Ni nini maana ya maisha?’.

Mwanzoni kabisa mwa msimulizi anakwambia kuwa ‘Soka lina maana kubwa kwenye maisha yako, naamini hivyo. Lakini maisha yako, historia yako na juhudi zako zina maana kwnye soka’.

Kwa ufupi tu Cantona ni shujaa wa maisha yake mwenyewe, moyo wake ulikuwa na majeraha mengi, alivuja jasho jingi na bado dunia ilimpuuza. Nitakwambia kwanini huko mbele na baadae ilikuaje.

Mbali na staili yake ya soka, kitu cha msingi tunachoweza kujifunza kutoka kwake ni namna mwanadamu anavyoweza kuishi na moyo wake.

Wakati mwingine Waswahili tunaamini kuwa kichaa anaweza kutembea umbali mrefu lakini safari yake akarejea na makopo, hilo limekuwa kinyume kwa kichaa Raheem Sterling.

Ndio, Sterling ni kichaa aliyesafiri umbali wa zaidi ya maili 5,000 kutoka katika kitongoji cha wanaharamu, wasaka fedha kwa mdomo wa risasi ndani ya Mji hatari wa Kingston, Jamaica.

Miaka zaidi ya mitano aliyoishi hapo, ilitosha kumfanya aubebe moyo wake kuanza ndoto za kusaka mafanikio nchini England

Ni pale katika mitaa ya Maverley, Jamaica, Sterling aliyashuhudia mauaji ya baba yake, ni katika mji huo, Raheem alipokuwa akijifunza soka huku pembeni vitendo haramu vya uporaji vikiendelea.

Hadithi yake ni mfano mzuri juu ya namna wazazi, shule na mpira vinavyoweza kuchanganyika na kuyatengeneza maisha ya kijana anayeweza kuiweka rekodi ya dunia kupitia kipaji chake.

Chris Beschi, mwalimu aliyemfundisha Sterling katika shule maalumu ya Vernon House, alisema siku ya kwanza alipoitazama sura ya Raheem aligundua kuwa kuna mengi yamezunguka katika kichwa chake yanayoweza kuizima ndoto iliyobebwa na miguu yake.

“Alikuja Vernon House kwa sababu alikuwa ameshindikana katika shule za kawaida, alikuwa na tabia mbovu. Kimtazamo alikuwa ni kijana mwenye uso wenye tumaini na tabasamu la faraja. Ni mtu mzuri akicheka, lakini huwa hatari pindi hasira zinapoutawala ubongo wake. Hapo hakuna aliyeweza kumsogelea!”

Beschi aliongeza: “Nakumbuka nilizungumza naye alipokuwa na miaka 10, nilimwambia, kama utaendelea kuishi na kufanya unachokifanya mpaka ukifika umri wa miaka 17, kuna mambo mawili yatakutokea, utakuwa mchezaji nyota wa England ama utakuwa umeshahukumiwa kifungo gerezani.

“Haikuwa kauli nzuri kwa kijana wa umri wake, lakini nafikiri hisia zangu zilinisukuma kuona ukweli ndio ungekuwa tiba kwake,” alimaliza Beschi.

Ilimlazimu Beschi kutembea umbali mrefu kila wiki, akimzungusha Raheem kwenye majumba ya kihistoria, wakipiga picha za kuvutia, lakini kwa bahati mbaya hapakuwa na dalili ya mabadiliko yoyote.

Raheem alikua anafanya utukutu wake dakika moja tangu baada ya kuimaliza safari yao. Ilichukua muda Sterling kubadilika, ikaja siku hii, mboni za macho yake zikaiona nuru ya uwanja wa Wembley ukipita mbele yake.

Ni siku hii alipotengeneza mechi ya vijana wahuni watano dhidi ya vijana wengine waliotokea St Raphael’s estate, Kaskazini Magharibi mwa jiji la London.

Mchezo ulipigwa katika viwanja vya shule ya Copland, karibu na uwanja wa Wembley. Ni siku hii, Raheem alipofurahia mchezo wa soka, ni siku hii maisha mapya ya Raheem yalipoanza.

Alipotimiza miaka 14, kwa mara ya kwanza Sterling akatokea katika kurasa ya mbele ya gazeti kubwa na maarufu Jamaica, gazeti la Gleaner. Habari yake ilishtua, kila aliyebeba gazeti aligoma kuamini yaliyoandikwa na sura ya Raheem wanayemfahamu. Muhuni!

Raheem alikuwa na ombi kwa vijana wa Jamaica kubadilika, kuachana na matukio ya kihuni yanayoichafua nchi yao. Katika kutia mkazo juu ya hilo, Sterling akaahidi kuichezea timu ya taifa ya Jamaica kama vijana wa nchi hiyo wakibadilika. Unadhani ilikuwa rahisi?

Sterling alirudi mwishoni mwa mwaka katika mitaa ya Maverley kwa ajili ya mazishi ya bibi yake. Kwa heshima na nembo yake ya kucheza soka Liverpool, Raheem alijumuika kucheza soka mtaani na vijana wenzake, pembezoni kidogo mwa nyumba yao karibu na barabara ya Reapers, eneo alilomshuhudia kijana wa miaka 15 akipigwa risasi na kufa mbele yao.

Hali ilikuwa ngumu hata katika shule ya Vernon ambapo kuna kipindi madarasani waliingia wanafunzi sita tu, wengine wangekuwa bize uwanjani kujifunza ujuzi wa soka katika miguu ya Raheem.

“Raheem alikuwa akicheza mpira saa mbili kila siku alipokuwa shule,” alisema Beschi. “Hakuwa wa ajabu sana, lakini alikuwa anajua namna ya kuutuliza mpira na kuulinda. Tukipokuwa tukipanga timu mbili zenye wachezaji 10, wakubwa wakiwa watano na wadogo watano. Timu iliyokuwa na Raheem ni kama ilikuwa na wakubwa sita,” aliongeza mwalimu huyo.

Mapema wiki hii, Paul Pogba na Rio Ferdinand walimzungumzia Sterling, kila mmoja anaamini hapewi heshima anayostahili kutokana na kiwango alichonacho sasa.

Katika umri wake wa miaka 24 yupo kwenye kiwango cha juu mno pengine kuliko Cristiano Ronaldo kwa wakati ule, Raheem anafunga na kutengeneza mabao, anapenda kucheza mpira wakati wote.

Achana na akina Sergio Aguero, Bernado Silva au Kelvin de Bruyne ndani ya kikosi cha Manchester City, imani ya Pep Guardiola yote ipo katika miguu ya Sterling, anamwamini kwa kila kitu.

Lakini siamini kama vyote hivyo vina uzito kwa Sterling kuliko maisha yake ambayo yalikuwa na milima mingi kuliko njia iliyonyooka anayotembea nayo sasa.

Ni katika umri wa miaka 17, Sterling alicheza mechi yake ya kwanza akiwa na jezi ya England dhidi ya Sweden mwaka 2012, wakati ambao alitabiriwa na Beschi kama hatokuwa nyuma ya nondo za gereza basi atakuwa mchezaji mahiri.

Wakati mwingine ni ngumu kuyaelewa maisha, Kazi imebaki kwake, anapata nafasi ya kuangalia nyuma na kugundua safari yake ilikuwa mbaya lakini mwisho wa siku furaha imemfuata kumaliza mwendo huo pamoja.

Ni pale pale kwa Cantona alipoamua kupambana kwa ajili ya kesho bora kwake na familia yake iliyokuwa ikihaha kila kukicha kukimbia kutokana na vita.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here