Home Makala ‘SUPER SUB GEDO’ MTU HATARI ALIYEACHA MTIHANI MGUMU KWA WASHAMBULIAJI AFRIKA

‘SUPER SUB GEDO’ MTU HATARI ALIYEACHA MTIHANI MGUMU KWA WASHAMBULIAJI AFRIKA

334
0
SHARE

LIBREVILLE, Gabon


MOHAMED Nagy ‘Gedo’. Kwa bahati mbaya huyu jamaa hakubahatika kuendeleza makali yake alipopewa nafasi ya kucheza soka la Ulaya. Baada ya kufanya mambo makubwa Afcon ya 2010 pale Angola na timu ya taifa ya Misri, miaka mitatu baadaye klabu ya Hull City ikamtoa nchini Misri na kumleta England.

Kila aliyeshuhudia makali ya Gedo, alikiri kabisa kwamba kiungo mshambuliaji huyo hatachukua muda mrefu kabla ya kuendeleza kile alichokianza Angola. Lakini kwa bahati mbaya presha ilimzidi.

Desemba 2009, mashabiki wengi wa soka hawakumjua Gedo ni binadamu wa aina gani alipojumuishwa kwenye kikosi cha awali cha Mafarao. Lakini baada ya kuonesha maajabu ndani ya wiki tatu za Afcon, jina lake lilizunguka kwenye vichwa vya hao hao walioguna kwa kuliona jina geni ndani ya kikosi cha Misri.

Alikuwa na miaka 26 tu kipindi hicho akiichezea klabu ya Al Ittihad, lakini njaa yake ya mabao ilimfanya awapiku kwa mabao mastaa wakubwa waliokuwepo kwenye michuano hiyo na kunyakua kiatu cha dhahabu.

Mabao matano tu yalitosha kwa yeye kunyakua kiatu hicho na kwa taarifa yako Gedo aliyatupia mabao yote hayo akitokea benchi. Kiufupi alikuwa ‘super sub’ ya hatari.

Balaa lake lilianza katika mchezo wa kwanza tu wa kundi C dhidi ya Nigeria, ambapo hadi kipindi cha pili Misri walikuwa wanaongoza mabao 2-1, alipoingia zikiwa zimebaki dakika chache mno mchezo kumalizika na akatupia bao lake la kwanza dakika ya 87. Bao lake la pili la hatua ya makundi alilifunga dhidi ya Msumbiji katika dakika ya 81 ya mchezo huo.

Kwenye hatua za mtoano ambazo zilikuwa na umuhimu mkubwa kwa Misri hadi walipofika fainali, Gedo aliendelea kufanya kazi moja tu, ya kufunga pale aionapo nafasi ya kufanya hivyo na dakika zake zile zile za lala salama.

Robo fainali dhidi ya Cameroon, alitupia bao la pili baada ya kutumia dakika chache akitokea benchi kwenye dakika 30 za nyongeza na kuisaidia timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 3-1. Na bao lake la nne la michuano lilikuja katika mtanange dhidi ya Algeria walioshinda mabao 4-0, akifunga kwenye dakika 90 na mbili za nyongeza.

Hapo ndipo jamii ya soka la Afrika na duniani kwa ujumla walipombatiza jina la ‘super sub’ kutokana na aina ya mabao aliyokuwa akiyafunga akitokea benchi.

Mchezo wa mwisho kwake kutupia bao lililompa kiatu cha dhahabu na kuweka rekodi ngumu ambayo zaidi ya kuvunjwa, haitakuja kufikiwa hivi karibuni na mshambuliaji wa Kiafrika, alilifunga kwenye fainali dhidi ya Ghana.

Gedo alifanya jambo jema kuikumbusha jamii ya soka kwamba mchezo ule usingekuwa mwepesi. Na kweli, tukaishuhudia fainali ngumu iliyosubiri maamuzi ya Gedo mwenyewe ambaye aliingia dakika za mwisho na kufunga bao pekee la ushindi dakika ya 85 na kuisaidia Misri kunyakua taji lao la tatu mfululizo mwaka huo.

Historia aliyoiandika mwaka huo ataikumbuka mno, kwani kuitwa kwake ili ajiunge na timu ya taifa kulikuja katika wakati asioutarajia na kwa wakati huo aliokuwa na mabao manne ndani ya mechi 12 kwa ngazi ya klabu, Gedo hakutegemea kama angeitwa.

Ule msemo wa umdhaniaye kumbe siye, ulitumika wazi kutuhukumu kwa kile tulichomfanyia Gedo 2010. Tulipodhani kwamba ni mchezaji mbovu kuitwa Misri, kumbe hakuwa yule tuliyemuwaza.

Alipata nafasi timu ya taifa baada ya makocha kuridhishwa na bao lake la shuti kali dhidi ya Mali jijini Dubai, Januari 4, 2010. Na hata bao hilo alilifunga akitokea benchi.

Nafasi nyingine zikamjia pale baadhi ya wachezaji muhimu wa Misri walipopata majeraha na kutokuwa fiti kwa ajili ya kucheza ambapo mchezo wa kwanza dhidi ya Nigeria wa Afcon kwa mara nyingine alipiga bao akitokea benchi na kuendelea hadi mchezo wa fainali.

Gedo alianza kucheza soka katika kituo cha watoto cha Hosh Essa na alipofikisha miaka 17, alijiunga na Ala’ab Damanhour, timu ndogo ya Ligi Daraja la Pili kabla ya kwenda Al- Ittihad Al-Sakndary mwaka 2005 na kuongeza mkataba mwingine hadi 2012.

Mabao matano ya Gedo yaliwapiku watu kama Ahmed Hassan (Misri), Flavio Amado wa Angola, Seydou Keita (Mali) na Asamoah Gyan (Ghana). Na kitu cha kushangaza ni kwamba, licha ya kuwa mastaa hao walianza na kumaliza dakika 90 za michezo yao, hawakuweza kufunga mabao kama Gedo alivyojua kutumia dakika chache kufanya makubwa uwanjani.

Gedo alifanya makubwa mno kwenye michuano hiyo licha ya kuwa walikuwepo washambuliaji hatari kama; Didier Drogba, Samuel Eto’o, Mohamed Zidan, Fredrick Kanoute, Yakubu Aiegbeni, Obafemi Martins. Aliibeba Misri kuandikisha rekodi ya mataji matatu mfululizo na kuliandika jina lake kwenye mchanga wa historia wa Angola.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here