Home Chombezo TAFUTA SABABU ZA KUACHWA KWAKO MARA KWA MARA

TAFUTA SABABU ZA KUACHWA KWAKO MARA KWA MARA

489
0
SHARE

NA JOSEPH SHALUWA,

MARAFIKI kwenye uhusiano, makosa fulani yakifanyika, ama kwa kujua au kwa bahati mbaya husababisha kupotea kwa furaha katika mapenzi.

Kwa bahati mbaya, baada ya kupoteza furaha ni vigumu kurudisha haraka. Hata kama ulikuwa na mwenzi mwingine kwa muda mrefu lakini baada ya kugundua matatizo yake na kuachana naye, utapata shida kupata mwingine.

Hata ukimpata ni vigumu kumzoea kwa muda mfupi, kuzoea mazingira na kujihakikishia kuwa ndiye mwenzi wako wa kudumu. Si ajabu  wapenzi kuachana, lakini inapotokea unakuwa wa kuachwa kila siku, lazima ujue kwamba kuna tatizo.

Ni jambo gumu kidogo kupata hekima ya kugundua jambo hili, lakini waliobahatika hufanya uamuzi ambao hauwaumizi mioyo yao. Haya mambo yanawezekana rafiki zangu.

Kwanza ni kukubali kujifunza, kuangalia wapi ulikosea, kipindi gani wenzi unaochana nao wanapatwa zaidi na hisia za kukuacha n.k. Baada ya hapo ni rahisi kusogea mbele zaidi katika kujua jinsi ya kutatua tatizo ulilonalo.

Wanawake wengi huhangaika kwa sababu ya kuachwa kila siku. Kila mwanamume anayekuwa naye baada ya muda mfupi tu anaachana naye! Hajui tatizo, badala yake anaishia kulia tu.

Kulia kwako hakutakusaidia lolote kama hutakaa chini na kujiuliza ni wapi kwenye matatizo, ni sehemu gani huwa unakosea!

Una miaka 24, lakini umeshakuwa na wanaume tisa! Hili ni tatizo, tena kubwa ambalo linahitaji dawa ya kuponya na si ya kutuliza maumivu.

Sikia kilio cha dada huyu: “Mpaka sasa nimechoka, nahisi kama sitakiwi kuwa na mpenzi, maana kila ninayekuwa naye lazima ananiacha. Neno nakupenda halina thamani kabisa katika maisha yangu ya sasa, yaani nimechanganyikiwa kabisa kaka Shaluwa. Utanisaidiaje niweze kupenda tena?”

Huyu ni Hilda (si jina lake halisi) wa Dar ambaye alipata kuzungumza nami ofisini kwangu hivi karibuni, jijini Dar es Salaam.

Kilio kama cha Hilda kipo kwa wanawake wengi sana nchini. Hilda  aliondoka akiwa mpya baada ya kuzungumza naye kwa takribani saa mbili.

Niliongea naye mambo mengi sana ambayo siwezi kuyaandika yote hapa, lakini kwa uchache sana pitia vipengele vifuatavyo vinaweza kukusaidia kukutoa kwenye tatizo hilo.

JICHUNGUZE, UNAJIRAHISISHA?

Kwanza jaribu kujichunguza kama una tabia ya kujirahisisha. Ni kweli umekuwa na tabia ya kujishusha thamani na kuona kama wewe ni wa kuonewa? Kuchezewa? Mwanamume mwenye ndoto na mwanamke wa baadaye wa maisha yake (mke) hahitaji mwanamke wa aina hii.

Anapenda zaidi awe na mwanamke mwenye msimamo anayetambua thamani yake yeye mwenyewe na maisha yake kwa ujumla. Hapendi mwanamke ‘maharage ya Mbeya’ maji mara moja!

Kama utakuwa wa aina hii, hata kama atakuwa amekupenda, ataishia kukutumia na kukuacha, kwani wewe mwenyewe umejionesha wa namna hiyo.

Mwanamume anapenda mwanamke wa kumsumbua kidogo, angalau baadaye apate stori za kusema: “Lakini mama nanilii ulinisumbua kukupata!”

Huu ni ukweli ambao baadhi ya watu wanaukwepa. Acha kujirahisisha. Kujirahisisha huku ni pamoja na suala zima la kukutana faragha, usiwe na haraka na tendo hilo, usiulizie juu ya hilo lakini kama ikitokea jamaa akataka, usikubali haraka. Onyesha msimamo wako, ukiainisha usivyotaka kuchezewa.

ANGALIA MIENENDO YAKO…

Wakati mwingine mambo yako yasiyotamanika yanaweza kuwa chanzo cha kuachwa na wenzi wako kila wakati. Angalia tabia zako, tazama mienendo yako, marafiki zako, kauli zako na kila kitu ambacho unadhani kinaweza kuwa tatizo.

Mwanamume hapendi kuwa na mwanamke ambaye ana kampani mbaya, kwani anaamini na wewe pia inawezekana ukawa na tabia chafu kama rafiki zako, lakini kauli nzuri kwa mwenzi pia ni kati ya mambo ambayo mwanamume mwenye nia ya kuoa atavutiwa navyo. Jiangalie upya!

 UNAJALI?

Kujiona wewe ni bora kuliko wanawake wote hakukusaidii, sana sana kunazidi kukurudisha kwenye matatizo yale yale kila siku. Mwanamke ambaye hajali na haonyeshi umakini wakati akizungumza na mpenzi wake, hana sifa ya kuwa mke.

Kama ni kweli unataka kuwa mke, lazima uwe makini, uonyeshe kujali kwako na kumwona mwenzi wako kila kitu. Mheshimu, mpe nafasi ya kwanza kwako, hiyo inaweza kuwa safari nzuri sana ya kuelekea kwenye mafanikio.

Jifunze unyenyekevu, ukikosea kuwa wa kwanza kuomba msamaha, kubali kusamehe na hakikisha kwamba unakubali kufundishwa unapokosea.

Usiwe mtu usiyejali, ambaye upo tayari kwa lolote, hata kama ni kuachana na mwenzi wako. Hii ni kati ya sumu hatari zitakazokufanya uishie kuachika kila siku.

KUNG’ANG’ANIA MAMBO

Tabia ya kung’ang’ania mambo ambayo mpenzi wako hapendi ni kati ya sababu zinazotosha kukufanya uachike. Inawezekana mpenzi wako  hapendi aina fulani ya mavazi, tabia fulani mbaya na amekuambia kwanini hapendi lakini wewe ukaendelea kung’ang’ania. Hilo ni tatizo.

Acha uking’ang’anizi, kuwa mwelewa. Mwenzi wako anapokataa kitu na kukueleza sababu za msingi, msikilize na kama unaona anachokuambia hakifai basi mjibu kwa hoja na si kumwekea kiburi.

DHARAU KUPINDUKIA

Wanawake wenye dharau wapo katika nafasi kubwa ya kuachwa na wapenzi wao. Utakuta mwingine dharau zake zinazidi mipaka mpaka kwa ndugu wa mpenzi wake. Wakigombana kidogo anaweza kutaja hata wazazi au ndugu wa karibu na mpenzi wake.

Ni mwanamume gani anayependa kuishi na mwanamke mwenye mdomo mchafu? Mwenye dharau? Anayeamini kila kitu anaweza mwenyewe?

Sifa ya kwanza ya mwanamke ni heshima, kama mwanamke huna heshima basi fahamu kwamba huwezi kuishi na mwanamume hata siku moja.

Katika maisha ya ndoa kati ya mambo ya msingi ambayo huzingatiwa na wengi ni pamoja na kila mmoja kukubalika na ndugu wa pande zote, sasa itawezekana vipi wewe kuolewa ikiwa hata hao ndugu wenyewe unawadharau? Unawadhalilisha kwa maneno makali? Itawezekana vipi?

Mwanamke lazima uwe na heshima, uwe na haiba ya kike, siyo unaishi mradi siku zinakwenda. Kama huwa unaachwa kila wakati, chunguza tabia hii nayo inaweza kuwa chanzo cha wewe kuachwa.

Wiki ijayo nitamalizia sehemu ya mwisho ya mada hii, usikose!

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here