SHARE

NA HENRY PAUL

UNAPOZUNGUMZIA miongoni mwa makipa mafundi wanaokumbukwa hapa nchini kutokana na uwezo mkubwa waliokuwa nao wakiwa langoni, kamwe huwezi kuacha kulitaja jina la Idd Pazi maarufu ëFatheríkama wapenzi wa soka walivyozoea kumwita.

Umahiri wa nyota huyu ndio uliomfanya mwaka 1983 kuwa kipa wa kwanza nchini kubatizwa jina la Tanzania One, huku mwaka 1980 akiwemo katika kikosi cha timu ya Taifa Stars kilichoshiriki michuano ya Mataifa Afrika kwa mara ya kwanza iliyofanyika mjini Lagos, Nigeria.

Mkongwe huyo pamoja na kuichezea timu ya Taifa Stars kwa mafanikio kwa kipindi kirefu, pia amezichezea klabu kadhaa zikiwemo Nyota ya Mtwara, Majimaji ya Songea, Simba, Pilsner, Al-Hilal ya Sudan, Wit Bank ya Afrika Kusini na Persija ya Indonesia.

Hivi karibuni DIMBA Jumatano lilifanya mahojiano na mkongwe huyo kutoa maoni yake kuhusiana na ushiriki wa timu ya Taifa Stars katika fainali za Mataifa Afrika zitakazofanyika nchini Misri kuanzia Juni 21 hadi Julai 19.

Katika mahojiano hayo Pazi ambaye alishiriki fainali za Afcon mwaka 1980, anatoa maoni yake akisema:

Pamoja na Taifa Stars kutokuwa na maandalizi ya muda mrefu, lakini ni matumaini yangu kuwa kwa sababu wachezaji wote wa timu hiyo walikuwa na timu zao katika ligi ambazo zimemalizika hivi karibuni, kama watajituma na kucheza kwa bidii wanaweza kufanya vizuri.

Kikosi cha timu ya Taifa Stars kilichochaguliwa hivi karibuni na kocha mkuu wa timu hiyo Emmanuel Amunike raia kutoka Nigeria, ni kizuri na chenye wachezaji mahiri na wenye vipaji vikubwa vya soka, hivyo wanaweza kuvunja rekodi yetu ya mwaka 1980.

Ikumbukwe kwamba mwaka 1980 wakati tunashiriki fainali hizo pamoja na kuwa na kikosi kizuri, lakini hatukufanya vizuri, kwani tulifungwa katika michezo mitatu na kupata sare mchezo mmoja.

Katika mchezo wa kwanza tulifungwa na wenyeji Nigeria mabao 3-1, mechi ya pili tulifungwa na Misri mabao 2-1 na mchezo wa mwisho tulitoka sare ya kufungana bao 1-1 na Ivory Coast.

Pamoja na kwamba mwaka huu timu ya Taifa Stars ipo katika kundi gumu na timu ya Kenya, Algeria na Senegal, lakini kutokana na kikosi chake kuwa na wachezaji wenye vipaji vikubwa vya soka wanaweza kufanya vizuri kama watacheza kwa bidii na kujituma.

Kwa upande mwingine timu ya Taifa Stars inaweza kufanya vizuri katika michuano hiyo kutokana na kuwa na wachezaji ambao wanangíara katika ligi za nje kama Mbwana Samata klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji, Simon Msuva anayechezea klabu ya Difaa El Jadid, Thomas Ulimwengu anayechezea klabu ya JS Saoura, Shaban Chilunda (Tenerife), Himid Mao (Petrojet), Rashid Mandawa (BDF XI) na Shiza Kichuya (ENPPI).

Nina imani kuwa wachezaji hao wanaowika katika ligi za nje, wakiungana na wachezaji wakongwe wanaocheza Ligi Kuu nchini kama John Bocco, Mudathir Yahaya, Kelvin Yondani, Feisal Salum, Jonas Mkude, Aggrey Morris na Gadiel Michael wanaweza kutoa ushindani kwa timu watakaoshindana nazo kama watacheza kwa kujituma.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here