Home Habari TAMBWE: SIMBA WAZURI, ILA YANGA MABINGWA TU

TAMBWE: SIMBA WAZURI, ILA YANGA MABINGWA TU

1331
0
SHARE

NA MAREGES NYAMAKA,

STRAIKA wa Yanga, Amissi Tambwe, mwishoni mwa wiki iliyopita alikaa mbele ya televisheni yake na kuutazama mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Ndanda FC ya Mbwara dhidi ya Simba ya Dar es Salaam na baada ya dakika 90 kumalizika Mnyama akiibuka kidedea, akakiri kuwa Wekundu hao wa Msimbazi ni balaa msimu huu, lakini wasahau kuhusu ubingwa.

Katika mchezo huo, uliopigwa katika dimba la Nangwanda Sijaona, Simba iliibuka mbabe kwa mabao 2-0 dhidi ya Ndanda, ambayo iliwalazimisha Yanga suluhu ya bila kufungana katika mechi yao iliyopigwa Septemba 7, mwaka huu kwenye uwanja huo huo.

Matokeo hayo ya Mnyama katika uwanja huo unaoelezwa kuwa ni mgumu kwa timu ngeni, yamemfanya Mrundi huyo kukiri kuwa Simba wako vizuri sana msimu huu katika mbio za ubingwa, lakini wao (Yanga) lazima watetee taji lao hilo.

“Simba wako vizuri kweli msimu huu, ukizingatia mchezo wao awali tena wa ugenini wamefanikiwa kushinda, hata ukiangalia kikosi chao kina wachezaji wenye viwango bora, ingawa kutwaa ubingwa wasahau hilo, lazima tutetee taji letu,” alisema Tambwe.

Tambwe amekuwa sehemu ya kikosi cha mafanikio cha Yanga tangu alipowasili mahali hapo akitokea kwa watani zao hao wa jadi, Simba, ambapo katika msimu uliopita, mabao yake ndiyo yaliyoiwezesha Yanga kutwaa ubingwa, huku yeye akiibuka mfungaji bora.

Wanajangwani hao wanatarajia kushuka dimbani Ijumaa wiki hii kuvaana na African Lyon, katika mchezo utakaopigwa Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here