SHARE

NA ZAINAB IDDY
KARIBU msomaji wa safu ya Filamu za Kibongo inayokujia kila siku ya Jumatano kupitia gazeti lako pendwa la Dimba.
Leo hii tunaingalia kazi inayoitwa ‘Tatoo’ iliyochezwa na wasanii Elizabeth Michael ‘Lulu au Brijet’, Ramadhan Miraji ‘Dastan’, Hasnat Mathius ‘Nicol’, Mandela Nicholaus ‘Neron’, Charles Magari ‘ Baba Nicol au Mzee Magali’, Grece Mapunda ‘Mama Dastan ‘ na wengine wengi.
Filamu hiyo inaanza kwa kumuonyesha binti wa mzee Magali akiwasiliana na mpenzi wake ‘Dastan’ ambaye amekuja kumchukua nyumbani wakapunge upepo ufukweni.
Lakini wakati wakijiandaa kuondoka mara anatokea Mzee Magali na kuanza kumfukuza Dastan huku binti yake akikimbilia ndani.
Katika kukimbia huku na huko Dastan anaanguka na kuumia, lakini anafanikiwa kurudi nyumbani kwao na kukutana na mama anayemkanya juu ya mahusiano yake ya kimapenzi na binti wa Magali.
Kule nyumbani kwa Mzee Magali baada ya kuingia ndani anampiga binti yake huku akimtaka kuachana na Dastan, kwa hasira Nicol anaingia ndani na kunywa sumu kwa lengo la kujiua.
Nicol anakimbizwa hospitali lakini kwa bahati mbaya madaktari wanaleta taarifa kuwa wameshindwa kuokoa maisha yake.
Lulu anampigia simu mama Dastan na kumpa taarifa ya msiba kwa lengo la kutaka amwambie mwanae naye anafanya kama alivyoambiwa.
Taarifa hizo zinamchanganya Dastan ambaye anaamua kwenda msibani huko anakutana na baba wa Nicol baada ya kumuona anamvamia na kumgongesha katika makaburi jambo linalo sababisha aumie kichwani na kupoteza kumbukumbu.
Madaktari wanajaribu kumtibia lakini wanashindwa na kuamua kumpeleka katika hospital ya vichaa na hiyo ni baada ya kuonekana amechanganyikiwa.
Nyumbani kwa mzee Magali nako hali inaonekana si shwari baina yake na kijana wake wa kiume Neron ambaye anaonyesha chuki ya wazi kwa baba yake sababu ikiwa kusababisha kifo cha dada yake Nicol.
Neron anaachukua maamuzi ya kuhama nyumbani kwao na kwenda kuishi kwa kipenzi chake Lulu, ambako huko wanapanga namna ya kurudisha kumbukumbu za Dastan.
Wawili hao wanakwenda kwa wachora tattoo na Lulu anachora ile ambayo Nicol aliwai kuchora kisha wanakubaliana ajifanye kichaa ili apate nafasi ya kukutana na Dastan mpango ambao wanamuhusisha na daktari mkuu wa kitengo cha vichaa.
Jambo hilo linafanikiwa kwani baada ya vituko vya hapa na pale, Lulu anapelekwa katika jumba la vichaa ambalo ndani yake Dastan anaishi na huko anafanya kila namna ya kurudisha fahamu zake kupitia ile tattoo.
Mara kwa mara Lulu anakwenda kukaa mbele ya Dastan na kuonyesha ile tattoo kitu ambacho kinaonekana kumvuruga Dastan kwani kuna matukio anayakumbuka ingawa si kwa asilimia 100.
Tukutane Jumatano ijayo kuona kama Lulu atafanikiwa mpango wake.
@@@@@@@@@@@@@@

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here