SHARE

NA NIHZRATH NTANI

NI takribani miaka 57 sasa tangu Juni 20, 1962. Muda umekwenda mno. Roho na mwili wake haupo nasi katika ulimwengu huu. Huku mwili wake ukiwa umepumzishwa katika mji wa Machui ulioko Kaskazini mwa Tanzania kunako Wilaya ya Tanga Mjini.

Nakiri sikupata kumwona hata wengi wetu hawakupata bahati ya kumwona na wale wachache waliobahatika kumwona wanaweza kukosa maneno sahihi ya kutuelezea kuhusu mtu huyu.

Mtu huyu anayesemekana ndiye baba wa lugha ya Kiswahili. Mwanamume huyu anayeelezwa kuwa ndio gwiji wa fasihi ya Kiswahili tuliyonayo hivi leo. Mtu huyu ni nani? Namzungumzia Shaaban Robert.

Shaaban Robert hayupo nasi kiroho hata kimwili. Hawezi kurejea tena lakini jina la Shaaban Robert bado linaendelea kuishi kwa miaka mingi zaidi mawazoni mwetu. Kwanini pamoja na kuondoka duniani bado jina lake linaendelea kuwa midomoni mwa Watanzania kizazi hadi kizazi?

Jibu ni moja tu. Alichokifanya enzi ya uhai wake hakiwezi kufutika kamwe. Mtunzi huyu wa vitabu ameacha alama isiyofutika milele na milele.

Alikuwa gwiji hasa wa mashairi, mtunzi wa riwaya na hata aliandika tamthiliya. Pengine watunzi wengi tulionao sasa ni chimbuko la kazi alizozifanya Shaaban Robert. Umeifanyia nini jamii yako? Jiulize. Upumzike kwa amani Shaaban Robert.

Usiku wa Novemba 22, 2014. Lionel Messi, alikuwa anavunja na kuweka rekodi mpya ya kufunga mabao mengi zaidi katika historia ya La Liga.

Wakati ‘hat trick” yake dhidi ya Sevilla ndani ya dimba la Nou Camp katika ushindi wa mabao 5-1 ilipoivunja rekodi iliyodumu kwa karibu miaka 60.

Ni jioni ya Oktoba 15, 2016. Ni Lionel Messi tena katika dimba la Nou Camp  alikuwa anavunja rekodi nyingine ya kuwa mchezaji aliyefunga magoli mengi zaidi katika La Liga kwa uwanja wa nyumbani dhidi ya Deportivo La Coruna.

Rekodi zote hizo anazozivunja Lionel Messi, ziliwekwa na mwanamume mmoja karibu miaka 63 iliyopita. Mwanamume huyu aliyeitwa Telmo Zarra.

Mwili wake ukiwa umepumzishwa huko katika ardhi ya makaburi ya Bilbao British karibu na Kijiji cha Sondika. Ni kilomita nane kutoka Kaskazini Mashariki mwa mji wa Bilbao ndani ya Jimbo la Basque.

Majina mengi yamepita kunako katika klabu ya Athletic Bilbao. Majina kama Guilermo Gorostika, Daniel Justa, Rafael “Pichichi” Equzkiza hata Agustin Gainza, lakini liko jina moja tu lingali linaimbwa na mashabiki katika dimba la San Mames. Ni Telmo Zarra.

 Zarra anatajwa kuwa ndiye mshambuliaji hatari zaidi aliyepata kutokea katika historia ya La Liga. Hakuna cha Alfredo Di Stefano, Hugo Sanchez, Cristiano Ronaldo wala Lionel Messi, aliyemvuka kwa takwimu. Ndio, nazungumzia kwa takwimu.

Ametumia misimu 15 katika La Liga akiichezea Athletic Bilbao. Akicheza mechi 277 na akifunga magoli 251 katika La Liga pekee. Lionel Messi, alihitaji mechi 289 kuvunja rekodi ya Telmo Zarra na kufunga magoli zaidi ya 251. Kwa hiyo Messi alicheza mechi 12 zaidi ya Telmo Zarra.

Aliweka rekodi ya kufunga mabao 179 katika mechi 167 akiwa uwanja wa nyumbani wa San Mames unaomilikiwa na Athletic Bilbao. Wakati Lionel Messi alihitaji mechi 176 kufunga magoli 180 akiwa Nou Camp.

Hayupo tena Telmo Zarra, lakini bado rekodi zake zinasubiriwa kuvunjwa katika soka la Uhispania. Bado rekodi yake ya kuwa mfungaji bora wa mashindano ya Copa Del Rey ya magoli 81 inaendelea kudumu kwa miaka mingi sasa.

Umahiri wa kutupia wa Lionel Messi na Cristiano Ronaldo (alipokuwa Hispania) bado haujaweza kumfunika Telmo Zarra.

Telmo Zarra alitwaa tuzo ya ufungaji bora wa La Liga mara sita kati ya mwaka 1944-1952, mpaka sasa hakuna aliyewahi kuvunja rekodi hii hata Lionel Messi. Tuzo ya Pichichi ilikuwa kama mali yake. Katika maisha yake akiwa na Athletic Bilbao.

Zarra alifunga jumla ya mabao 335 katika mechi 351. Ni tofauti ya mechi 19. Akicheza na kufunga magoli hayo katika mashindano mawili ya La Liga na Copa Del Rey tu.

KUIBUKA KWAKE KULISHANGAZA

Pamoja na kutajwa kuwa ndiye mshambuliaji hatari zaidi katika historia ya soka la Hispania. Historia ya Zarra kujiunga na mchezo wa soka inashangaza.

Baba yake aliitwa Telmo Zarra pia ambaye alikuwa injinia wa stesheni ya treni ya Asua na mama yake aliitwa Tomasa Montoya.

Telmo Zarra Jr alizaliwa katika familia ya watoto 10 huku yeye akiwa mtoto wa saba. Wakike watano na wa kiume watano. Baba yake Telmo Zarra Jr hakupenda mtoto wake awe mwanasoka.

Baba yake hakuona faida ya watoto wake kujiingiza katika soka. Baada ya kuwaona watoto wake wawili ambao walikuwa wakubwa zaidi ya Telmo Zarra.

Hata hivyo, Telmo Zarra, alikuwa anatoroka na kwenda kucheza na watoto wenzake huko mitaani. Mpaka pale alipoonekana ana kipaji kikubwa cha soka na kuonwa na klabu ya S.D Erandio iliyokuwa Second Division ligi ya tatu kwa ukubwa baada ya La Liga na Segunda Division.

Kutua kwake Athletic Bilbao kulikuja kama bahati. Ni baada ya Zarra kuchaguliwa katika timu ya mkoa ya Biscay iliyocheza mechi ya kirafiki na timu ya Guipuzcoa na Biscay kushinda goli 9-0 huku Zarra akitupia goli 7 peke yake.

Miaka 2 baadaye Telmo Zarra, alijiunga na Athletic Club. Ni mahala hapo ndipo alipoweza kuacha historia kubwa isiyofutika na inayodumu mpaka hivi leo. Jina lake linabakia kuimbwa mithili ya mfalme kunako klabu ya Athletic Bilbao.

Alifariki Februari 23, 2006 akiwa na miaka 85 kwa shinikizo la moyo. Pamoja ya kuwa hayupo duniani tena alichokifanya katika soka la Hispania bado kitaendelea kukumbukwa kwa miaka mingi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here