Home Michezo Kimataifa TFF ‘ILIVYOWAPOTEZA’ MANARA, MURO

TFF ‘ILIVYOWAPOTEZA’ MANARA, MURO

378
0
SHARE

NA SALMA MPELI,

HIVI karibuni tumeshuhudia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likimfungia Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, kujihusisha na masuala ya soka ndani na nje ya nchi kutokana na makosa ya kimaadili.

TFF kupitia Kamati ya Nidhamu, imemfungia Manara mwaka mmoja kutojihusisha na masuala ya soka pamoja na kumpiga faini ya Sh milioni 9 kutokana na makosa mbalimbali.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu, Wakili Jerome Msemwa, alisema kwamba hatua hiyo imefikiwa baada ya Manara kukutwa na makosa matatu dhidi ya TFF waliomlalamikia.

Kosa la kwanza ameamuliwa kulipa Sh milioni 1, kosa la pili atalipa Sh milioni 3 na la tatu Sh milioni 5, hivyo kufanya jumla kuwa milioni 9 kwa makosa yote hayo.

Msemwa ameyataja makosa hayo ya Manara dhidi ya mlalamikaji, TFF kuwa ni kuituhumu na kuidhalilisha TFF, kueneza chuki za ukabila na la tatu kuingilia utendaji wa shirikisho hilo.

Kwa makosa hayo yote, anakumbana na adhabu ya kuwa nje ya masuala ya soka kwa mwaka mmoja na kulipa faini ya Sh milioni 9 kabla ya kumaliza adhabu yake.

Lakini jambo hilo si geni katika soka nchini, kwani wapo wadau mbalimbali nchini waliofungiwa na shirikisho hilo kutokana na sababu mbalimbali.

Msimu uliopita, TFF kupitia Kamati hiyo hiyo, ilimfungia mwaka mmoja na faini ya Sh milioni 3 Mkuu wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro.

Kamati hiyo chini ya Wakili Wilson, ilimsimamisha Muro kutokana na kile kinachodaiwa ni kudharau maamuzi ya Kamati ya Nidhamu ya TFF mwaka 2015 alipoamriwa kulipa faini ya Sh milioni 5 alipokutwa na hatia na kutolipa fedha hizo, kitu ambacho taarifa ya Mwenyekiti wa Yanga alibainisha kuwa ilishalipwa.

Mengine yaliyomsulubu Muro ni yale yaliyohusu kuelekea mechi ya mashindano ya CAF ya Kombe la Shirikisho ambayo Yanga waliamua mechi hiyo iwe bure kwa mashabiki wote.

Muro amebakisha miezi kadhaa kumaliza adhabu yake hiyo, lakini hata hivyo, hadi sasa Muro ni kama amepotezwa kabisa kutokana na adhabu hiyo, kwani amesahaulika katika dira ya soka nchini.

Hofu ni kwamba, hali hiyo pia itakwenda kumkuta Manara katika muda wote atakaokuwa anatumikia adhabu yake hiyo.

Licha ya wawili hao kukutwa na hatia na kufungiwa na TFF, kwa kiasi fulani watakuwa wamepoteza ile ladha ya soka, hasa kwa mashabiki wa timu za Simba na Yanga.

Muro na Manara sasa hawatasikika tena katika medani ya soka kutokana na kufungiwa huko, lakini ikumbukwe pia mbali na wasemaji hao wawili kufungiwa na TFF, lakini pia Shirikisho hilo si mara yake ya kwanza kutoa adhabu kama hiyo.

Ni wazi kuwa, adhabu ya kumfungia Manara na kutakiwa kulipa faini ya Sh milioni 9, uhenda zikamfanya msemaji huyo wa zamani wa Simba kutoonekana tena wala kusikika akitoa mchango na mawazo yake katika mchezo wa mpira wa miguu.

Ikumbukwe kuwa, mbali na kuwa alikuwa msemaji wa Simba, lakini ni miongoni mwa watu ambao Taifa la Tanzania lilikuwa bado linahitaji mchango wake katika mustakabali mzima wa kulikuza soka la hapa nchini.

Mdau msomi, Damas Ndumbaro, pia ni miongoni mwa watu waliokumbana na adhabu ya kufungiwa kujihusisha na masuala ya soka kwa muda wa miaka 7.

Wengine ni aliyekuwa kocha msaidizi wa timu ya Geita, Choke Abeid (maisha), kipa wa Geita Mohamed Mohamed  (miaka 10), Yusuph Kitumbo na Fateh Remtula (maisha), huku waamuzi Masoud Mkelemi, Fedaian Machunde nao wakikumbana na adhabu kama hiyo.

Nachelea kusema kurudi tena kundini katika masuala ya soka kwa Muro na Manara hivi sasa kutategemeana na viongozi wapya wajao wa TFF, mara baada ya kufanyika uchaguzi mkuu wa Shirikisho hilo Agosti mwaka huu.

Endapo TFF viongozi wapya watafanikiwa kuingia na kuwang’oa akina Malinzi, ni wazi kuwa Manara na Muro tunaweza kuwasikia tena endapo watapewa msamaha, lakini vinginevyo adhabu walizopewa vijana hao ni kubwa na zimelenga kuwamaliza kabisa katika kutoa mchango wao kwenye mchezo wa soka.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here